Thursday, 19 October 2017

KAMANDA WA POLISI MKOA WA TANGA,WAKULYAMBA AKIZUNGUMZIA JINSI ALIVYOFANIKIWA KUTATUA MGOMO WA DALADALA NA MIKAKATI ILIYOPO KWA JESHI LA POLISI KATIKA KUSIMAMIA SHERIA YA USALAMA BARABARANI,,,

Pichani ambaye amevaa shati la kitenge ni kamanda wa polisi mkoa wa Tanga,Benedict Wakulyamba mara baada ya kikao kutatua mgomo wa waendesha daladala ukumbi wa bwalo la polisi mkoani hapo,akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani) jinsi ulivyotatuli na changamoto zilizopelekea kujitokeza na mikakati iliyopo.
 Pichani ni miongoni mwa madereva na makondakta wa daladala jijini Tanga wakiendezha mgomo eneo la Komesho mabawa jijini hapo.
Pichani ni miongoni mwa madereva wa daladala jijini Tanga wakizungumza na waandishi wa habari ambao (hawapo pichani) kilichopelekea kugoma kutoa huduma ya usafirishaji kwa wananchi.

NA SOPHIA WAKATI,TANGA
MADEREVA wa wanaoendesha magari madogo ya abiria maarufu 'Daladala' Jijini Tanga, wameanza mgomo jana wa kusitisha huduma ya usafiri katika Jiji hilo,wakidai kwamba kumekuwepo na ongezeko la utozwaji wa faini za makosa mbalimbali kunakofanywa na askari wa usalama barabarani hatua ambayo inawasababisha washindwe kutoa huduma kwa wananchi.
Lakini, wakati madereva hao wakiwa wamegoma na kujikusanya katika eneo la chuo cha biashara maarufu Komesho, askari wa kituo cha polisi Chumbageni wakiongozwa na Mkuu wa Upelelezi wa wilaya ya Tanga OCID Jumanne Njoka, waliwatawanya kwa kuwapiga mabomu ya machozi wakidai mkusanyiko huo haukuwa halali.
Kablya ya kupigwa mabomu hayo baadhi ya madereva walikuwa wameondoka na Mkuu wa Kituo cha Usalama Barabarani Abel Nyaleja, kuzungumzia mgomo huo na hatua ambazo watazichukua lakini hata hivyo kikao chao kiliairishwa hadi Jumatano watakapokuwepo viongozi wakuu wa jeshi hilo na viongozi wengine.

Wakizungumza na gazeti hili baadhi ya madereva hao wamesema mgomo huo ulioanza jana asubuhi, utadumu hadi Jumatano ambako kutakuwa na kikao baina ya madereva na wamiliki, Mamlaka ya Mapato (TRA), Mamlaka ya Udhibiti wa usafiri wa majini na nchi kavu (SUMATRA), Mkurugenzi wa Jiji la Tanga na Mkuu wa kikosi cha Usalama Barabarani, kikao chenye lengo la kupata muafaka wa namna bora ya utoaji huduma ya usafiri huo.

Dereva wa daladala inayofanya safari kati ya Raskazone hadi Mwahako, Said Waziri, aliainisha makosa ambayo yamekuwa yakitokeza mara kwa mara kuwa ni pamoja na kukamatwa pindi wanaposhusha abiria katika maeneo mbalimbali ya Jiji hilo hasa barabara za namba ambako wanaelezwa kwamba hakuna vituo.

Suala jingine alisema kuwa ni pale unapopakia katika kituo cha daladala ambacho zamani ilikuwa ni kituo cha mabasi yaendeyo mikoani, lakini ukitaka kutoka kabla hawajatoka na kumetokea abiria wakifungua mlango kumpakia askari anayekaa kwenye kibanda kilichopo ene hilo huandika kosa na wakati mwingine hushusha abiria wote.

"Kiukweli sasa hivikazi hii ya daladala haiwezekani tena, unakuta trafick (askari wa usalama barabarani) anakukamata kosa labda anasema gari bovu lakini anakuandikia makosa matatu ulipe sha 90,000 hadi sh 120,000 kwa kazi hizi hizo fedha tutazipata wapi na tajiri hesabu yake nampelekea nini, mimi watoto wangu watakula nini bado mmiliki anatakiwa kuliko kodi ya mapato," alisema dereva mwingine aliyejitabulisha kwa jina la Bakari Kizinga.

Mmiliki mmoja mwenye daladala zinazokwenda Donge/Raskazone na Mikanjuni/Stendi Mpya, Aisha Chabai alisema kuwa wao kama wamiliki mgogoro huo wa daladala hizo na askari wa usalama barabarani walishauwasilisha kwa mtu aliyemtaja kuwa na Mwnyekiti wa Chama Cha wasafirishaji wa daladala (MUWATA) aliyemtaja kwa jina moja la Atwabi lakini hakuna suluhu yoyote hadi madereva walipogoma jana.

"Kiukweli sisi wamiliki wa daladala kwanza hatuna imani na Atwabi (Shaabani) kwa maana tatizo hili tulilizungumza muda mrefu pengine lingepata ufumbuzi haya yasingetokea leo huu mgomo suingekuwepo...Sisi tunaungana na madereva wetu kwamba suala hili lipatiwe ufumbuzi maana hata tukitaka daladala zifanye kazi madereva ni hawa ambao wamegoma,"alisema Chabai na kuiomba serikali ilishughulikie suala hili.

Mmiliki mwingine Azizi Jafar mwenye daladala linalokwenda Tanga Beach/ Raskazone, aliiomba serikali kulitafutia ufumbuzi suala la mgomo huo kwa maana kwamba limekuwa likiathiri kipato cha madereva wanaoendesha magari hayo lakini pia linasababisha kero kwa wafanyakazi, wanafunzi wanaowahi kazini kufanya kazi.

"Sisi tunalipa kodi ya mapato, tunalipa Jiji TRA, SUMATRA sasa tunaposimaisha kazi kama hivi mapato yanakosekana lakini pia hawa vijana wanaathirika na familia zao na abiria ambao ni wafanyakazi na wanafunzi wanachelwa kufika kazini na shule, tutatue mzozo huu hakuna dereva anayetaka kuvunja sheria za usalama barabarani lakini askari wetu nao watazame makosa mengine," alisema mmiliki mwingine Said Zimbwe na kudai kwamba Atwabi hana daladala hivyo amepoteza sifa za kuwa kiongozi wa wasafirishaji.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa MUWATA Shaaban Atwabi alikiri kweli kwamba hana daladala kwa sasa baada ya daladala aliyokuwa akimiliki awali kuharibika lakini kwa vile ni mwasisi wa uanzishwaji wa usafiri huo analazmika kusimamia na kufanya shughuli zote za chama hicho ambapo suala la mgomo tayari ameanza kulishughulikia.

Ofisa Mkuu wa SUMATRA mkoani Tanga, Dkt Walukani Luhamba, alikiri kuwepo kwa mgomo huo na kwamba kiasi cha aslimia 75 cha daladala katika maeneo ya mjini yamegoma kwa kulalamika kuhusu madai ya kuongezeka kwa utozwaji wa faini unaofanywa na kikosi cha usalama barabarani hatua ambayo amedai viongozi wameanza kuyashughulikia.

Baadhi ya wananchi wakizungumzia mgomo huo walisema kwamba umeleta usumbufu mkubwa asubuhi kutokana na kukosekana kwa daldala hizo katika maeneo mbalimbali ya Jiji hili na hivyo kuchelewa kufika kazini na kwamba ni vema serikali ikatazama suala hilo.

Mwenyekiti wa Mtaaa wa Mapinduzi Jijini Tanga Athumani Mganga, alisema kwamba katika maeneo ya Magomeni hasa eneo la Komesho, alikuta wananchi wengine wakiwemo wanafunzi wakisubiri daladala hizo bila mafanikio na wengine walianza kutembea kwa miguu.

Kamanda wa Polisi Mkoani Tanga, Benedict Wakulyamba, ambaye jana wakati mgomo huo ukitokea alikuwa Amani wilayani Muheza na Mkuu wa mkoa wa wakimwakilisha Waziri wa Maji Injinia Isack Kamwelwe kwenye uzinduzi wa kamati za maji.

Alisema kuwa suala hilo linashughulikiwa na litarejea katika hali yake ya kawaida lakini aliwataka maderva lazima watii sheria bila shuruti kupunguza ajali za makosa yanayoweza kujitokeza barabarani.
Mwisho.


 

No comments:

Post a Comment