Monday 6 May 2024

DC HANDENI,WAKILI MSANDO AWAASA WAHITIMU MGAMBO JKT WAKAEPUKE KUSHAWISHIWA KUJIINGIZA KWENYE VITENDO VYA UHALIFU,,,


Pichani ni Mkuu wa wilaya ya Handeni,Wakili Albert Msando akiwaasa wahitimu katika hafla ya kufunga mafunzo kambi ya Mgambo kikosi cha 835 KJ kilichopo Kabuku wilayani Handeni mkoani Tanga.

NA SOPHIA WAKATI,HANDENI
WAHITIMU mafunzo ya Operesheni ya miaka 60 kujitolea kujenga taifa kikosi cha Mgambo JKT iliyopo wilayani Handeni wametakiwa kuyatumia vema mafunzo waliyopata huku wakiepuka kudanganywa kwa kushawishiwa ili kujiepusha kuingia kwenye vitendo vya uhalifu na hivyo kulisaliti Taifa lao.

Ushauri huo umetolewa na Mkuu wa wilaya ya Handeni,Wakili Albert Msando alipokuwa mgeni rasmi katika hafla ya kufunga mafunzo ya awali kwa wahitimu wa Mgambo JKT kikosi cha 835 KJ kilichopo Kabuku wilayani Handeni mkoani hapa.

Wakili Msando aliwaasa wahitimu hao akisema,wanapaswa kutumia vizuri mafunzo waliyopata na akiwasisitiza uadilifu na kukiishi kiapo walichoapa huku wakijilinda kwa kuepuka kushawishiwa na kutumikia kwenye uhalifu. 

Alisema, vijana hao ambao ni jeshi la akiba wanategemewa kuwa walinzi wazuri wa Taifa lao na kwamba itapendeza wakiepuka kuingizwa kwenye ushiriki wa vitendo viovu na kwamba atakayediriki kufanya hivyo sheria haitasita kuchukua mkondo wake.

Aidha Msando amewaasa vijana hao juu ya matumizi bora ya mtandao akisema ukuaji wa teknolojia umesababisha watu wengi kuingia kwenye matumizi ya Simu selula ambapo wengine wamekuwa wakitumia vibaya na wengine vizuri.

Amesema,wahitimu wa Mgambo JKT wanapaswa kutumia vizuri teknolojia ili iweze kuwanufaisha katika maisha yao huku Taifa nalo likiweza kupata faida badala ya kuitumia visivyo.

"Tuwe makini katika matumizi ya mitandao tutumie kwa faida zetu na Taifa letu"alisema Wakili Msando huku akishauri wahitimu hao wa mafunzo ya awali JKT kwa kujitolea kuendelea kulelewa badala ya kuachwa wenyewe.

Aidha ametumia nafasi hiyo kwa kuzishauri halmashauri za wilaya kuangalia uwezekano wa kuwatumia vijana hawa katika eneo la ukusanyaji mapato akisema Handeni ilishaanza kufanya hivyo na imepata mafanikio makubwa baada ya kufanikiwa kukusanya kwa asilimia 109 huku mwaka wa fedha ukiwa haujaisha.

Naye Mwakilishi wa Mkuu wa Majeshi Kanali Ernest Elias amewapongeza vijana hao wahitimu kwa kuitikia wito na kujituma kupokea mafunzo hadi kuweza kufikia katika viwango bora.

Alibainisha kuwa Serikali inaendelea kufanya maboresho imetoa fedha kiasi cha Shilingi million 570 zilizowezesha kuimarishwa kwa miundombinu hali ambayo imesababisha vijana wengi kupata nafasi ya kujiunga na kikosi cha Mgambo JKT.

''Tunaishukuru serikal inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha nyingi million 570 kwenye kambi ya Mgambo JKT,kuwezesha kufanya maboresho ya mabweni kuwezesha kupokea vijana wengi zaidi ya 900''Alisema Mwakilishi huyo wa mkuu wa Majeshi.

Awali,Kamanda wa kikosi cha Mgambo JKT,Lutten Kanal Raimond Hafrey Mwanry alisema kwamba vijana hao walianza kujiunga na mafunzo yao Desemba 27 mwaka 2023 ambapo wameiva na wako tayari kulitumikia taifa lao.
Mwisho.






 

Tuesday 30 April 2024

MAHAFALI YA 64 CHUO CHA UALIM KOROGWE MKOANI TANGA YALIKUWA HIVI 2024,

Pichani ni miongoni mwa wahitimu wa chuo cha ualim Korogwe siku ya mahafali.

NA SOPHIA WAKATI,KOROGWE
SERIKALI ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt.  Samia Suluhu Hassan imetoa mikopo zaidi ya Shilingi million 40 za kitanzania  kwa wanafunzi wa Chuo cha Ualimu Korogwe, Mkuu wa Chuo hicho cha, Hassan Abdillah Ismail ameeleza.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa chuo cha Ualimu Korogwe,Abdilah Ismail ametoa taarifa hiyo wakati akizungumza kwenye mahafali ya Wahitimu 259 wa stashahada ya Ualimu ambapo alisema fedha hizo tayari zimeshakabidhiwa kwa wanafunzi husika.

Ismail amewasilisha shukrani zake kwa Serikali kutokana na hatua yake hiyo ya kuwezesha mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vya ualimu na vile vya kati jambo ambalo hapo awali halikuwahi kuwepo.

Aidha Mkuu huyo wa chuo cha ualimu alisema, mitihani kwa wahitimu hao wote inatarajiwa kuanza Mei 6 mwaka huu huku wanafunzi hao wakiwa wamesoma masomo ya Sayansi ili kuwa walimu wa sekondari na kwamba wameandaliwa vizuri kitaaluma na kimaadili.

Kwa uoande wake Kaimu afisa elimu idara ya elimu Sekondari katika Halmashauri ya Mji Korogwe, Omari Mlawa aliwashauri wahitimu hao kwenda kujishughulisha na kilimo na ujasiriamali wakati wakisubiri ajira zao.

Alisema,licha ya kufahamika uwepo wa changamoto ya ajira,wahitimu hao hawapaswi kusubiri ajira badala yake wakajikite kwenye kilimo na ujasiriamali ili kuweza kujikwamua kiuchumi.

Pamoja na hayo, Mlawa alisema kwamba Halmashauri ya Mji Korogwe imejipanga kuwatumia wahitimu hao katika shule zilizopo kwa mtindo wa kujitolea huku wakiwalipa kiasi kidogo cha fedha za Sabuni. 

Aidha,aliwashauri wahitimu hao kutokusita kuwasilisha barua zao za maombi ya ajira za kujitolea kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe ili kuweza kupata fursa hiyo ya kufundisha.

Katika risala ya wahitimu wa Stashahada ya Ualimu iliyosimwa na Sharon Faustin Shaigwa alisema, chuo kinakabiliwa na changamoto udogo wa maabara ya Tehama ikilinganishwa na idadi kubwa ya wanafunzi.

Changamoto nyingine ni uchakavu wa miundombinu ya maji taka,kukosa uzio,ukosefu wa daktari, uhaba wa samani na upungufu wa vifaa tiba.
Mwisho.


Wahitimu.

Pichani ni Rais wa wanafunzi chuo hicho,Sharon Faustin ni miongoni mwa  wahitimu wanaomaliza masomo yao huku akishiriki Mahafali ya 64 kwa niaba ya wenzake ameahidi kwenda kuitumia vyema taaluma waliyopata na kwamba watafanya kazi kwa bidii kupitia nyanja mbalimbali ikiwa sehemu ya mafunzo waliyoyapata chuo cha ualimu Korogwe.


Pichani ni miongoni mwa wahitimu ,Husna  Benjamin amesema ataenda kutumia taaluma yake kwenda kuelimisha jamii na watu waamini hakuna kitu kigumu katika maisha na kuiomba serikal kutoa ajira.

Wahitimu wa chuo hicho.





 

Sunday 28 April 2024

TAKUKURU MKOANI TANGA JINSI ILIVYOFANIKIWA KUOKOA SHILINGI 439,279,300 ZA MAREJESHO YA MIKOPO KUTOKA KWA WANUFAIKA,

Pichani ni Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Tanga,Victor Swella akitoa taarifa kwa waandishi wa habari mkoani Tanga juu ya utendaji kazi wao kwa kipindi cha Januari hadi Machi 2024.

NA SOPHIA WAKATI,TANGA
TAASISI ya Kuzuia na kupambana na Rushwa TAKUKURU Mkoa wa Tanga imeokoa kiasi cha Shilingi 439,279,300 za kitanzania ikiwa ni fedha za marejesho kutoka kwa wanufaika wa mikopo ya asilimi 10% katika halmashauri ya Jiji Tanga. 

Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Tanga,Victor Swella aliyasema hayo Aprili 25 wakati alipokuwa akitoa taarifa kwa Umma kupitia vyombo vya habari juu ya utendaji kazi wao kwa kipindi cha Januari hadi Machi 2024.

Katika taarifa yake hiyo, Swella alisema, miongoni mwa kazi zilizofanywa na TAKUKURU kwa kipindi cha Januari - Machi 2024 ni ufuatiliaji wa ufanisi kwenye utekelezaji mkakati utoaji mikopo ya asilimia 10 kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu. 

Alisema kwamba,moja ya mambo yaliyobainika kwenye ufuatiliaji huo ni kutokuzingatiwa kwa masharti ya urejeshaji wa mikopo hiyo kwa wakati kutoka kwa Wanufaika.

Swella alibaisha kuwa, kabla ya ufuatiliaji kufanyika kiasi cha Shilingi 2,152,229,900 zilikuwa hazijarejeshwa kutoka kwa wanufaika wa mikopo hiyo huku muda wa kufanya marejesho ukiwa umepita.

Alisema kwamba, Takukuru baada ya kubaini hali hiyo,iliwakutanisha wadau na kuweka mapendekezo ya kurejesha fedha hizo na hadi kufikia Februari 2024 Shilingi 439,279,300.00 zilirejeshwa katika Halmashauri ya Jiji la Tanga na kufanya fedha zisizorejeshwa kuwa Shilingi 1,712,950,600.00.

Kuhusu Programu ya Takukuru Rafiki Mkoani Tanga, Swella alisema katika utekelezaji wameweza kuzifikia Kata 25, kero 284 zikitambuliwa na kuchambuliwa ambapo kero 163 zimetatuliwa na kero 121 zipo katika hatua mbalimbali za utatuzi. 

Pia taasisi hiyo ya kuzuia na kupambana na rushwa Takukuru, imeendelea na kufanya ufuatiliaji utekelezaji wa miradi ya maendeleo 46 iliyogharimu Shilingi 8,041,998,680.00 kwenye sekta za kipaumbele elimu, maji, afya na barabara. 

Katika ufuatiliaji huo, miradi 22 yenye thamani ya Shs. 4,866,068,966.00 ilibainika kuwa na mapungufu na ushauri umetolewa wa kuweza kurekebisha mapungufu hayo kupitia vikao vya wadau husika huku uchunguzi ukianzishwa kwa miradi ambayo ilibainika uwepo wa tuhuma za rushwa.

Miongoni mwa miradi inayochunguzwa ni manunuzi ya Shilingi. 6,400,000.00 ya uwekaji milango kwenye mradi wa ujenzi nyumba za wakuu wa idara katika Halmashauri ya wilaya ya Korogwe uliogharimu Shilingi 245,000,000.00.

Mradi mwingine ni ujenzi wa madarasa mawili, matundu 18 ya vyoo na mfumo wa uvunaji maji ya mvua uliyogharimu Shilingi 70,000,000.00 na uchunguzi unaofanyika ni ubadhilifu wa Shilingi. 30,000 000 ujenzi wa matundu 18 ya vyoo na mfumo wa uvunaji maji ya mvua.

Kwa upande wa uelimishaji, Mkuu huyo wa Takukuru Mkoa wa Tanga alisema,katika utekelezaji jukumu hilo wamewafikia wananchi 586,485 kupitia mikutano ya hadhara 39.

Vilevile kumefanyika maonesho 11, wanafunzi wa shule na vyuo wanaofikia 28,364 kupitia uimarishaji klabu 70 za wapinga rushwa, pia makundi wadau watoa huduma yamefikiwa wakiwemo watumishi 1975 wa sekta binafsi na waliojiajiri katika fani mbalimbali zinazohusika na huduma za jamii.
Mwisho

Sunday 3 March 2024

UZINDUZI WA NYUMBA 23 KWA AJILI YA MAKAZI YA KUDUMU KWA WATOTO YATMA ILIKUWA HIVI 2024,,



Pichani katikati ni Meya wa halmashauri ya Jiji la Tanga, Abdarahman Shilloo akikata utepe hafla ya nyumba 23 kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga,Waziri Kindamba.. 

NA SOPHIA WAKATI,TANGA
WATOTO Yatima 51 katika Halmashauri ya Jiji la Tanga wamenufaika na mradi wa Ujenzi Nyumba za makazi uliogharimu kiasi cha shilingi 652,000,000 Milioni hadi kukamilika.

 Meya wa Jiji la Tanga, Abdarahman Shilloo akikabidhi vyeti vya nyumba hizo 23 kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga,Waziri Kindamba alisema ni jambo jema kwa jamii na serikal. 

Alisema Ujenzi wa nyumba hizo uliofanyika eneo la Bagamoyo mtaa wa Amani na Kilimani kata ya Tangasisi, ni matokeo ya ufadhili wa Waterfall Charity UK huku usimamizi ujenzi ukifanywa na taasisi ya Masjid Muzdalifa ya Jijini Tanga. 

Akizungumza baada ya kukabidhi hati za nyumba hizo kwa Yatima, Meya Shilloo amewapongeza Waterfall Charity UK kwa ufadhili na Masjid Muzdalifa kwa kusimamia kazi kwa uadilifu hadi kukamilika ujenzi wa makazi hayo.

"Bila Muzdalifa Waterfall isingefanya chochote. Imesimamia kazi kwa uadilifu na uangalifu mkubwa"alisema Shilloo huku akitanabaisha kuwa ni taasisi chache zenye uwezo kama ule wa Muzdalifa. 

Aidha amewataka Muzdalifa kuendelea na uaminifu wao hatua ambayo itawawezesha kuwa kiungo muhimu kati yao na jamii katika kuisaidia Serikali kwa maelezo kuwa majukumu yanayoikabili ni mengi hivyo inahitaji taasisi zenye kuzingatia uadilifu. 

Naye Katibu wa Masjid Muzdalifa,Twahir Twaha aliyemwakilisha Mkurugenzi wake Twaha Tawakal amewashukuru Waterfall Charity UK kwa ushirikiano waliouonesha hadi kufanikisha upatikanaji nyumba za watoto Yatima. 

Twaha alisema,uhitaji wa nyumba hizo ulionekana katika kipindi ambacho barabara ya Pangani Tanga ilikuwa ikipanuliwa kwa nyumba zilizopo jirani kubomolewa kupisha ujenzi.

"Mahitaji tuliyaona kupitia madarasani wanafunzi wetu wanaosoma walivyokuwa wakitaabika hapo tukagundua changamoto ya walezi kukosa makazi na tukawaomba Waterfall Charity UK kusaidia"alisema Twahir Twaha Tawakal. 

Twahir aliwaomba wadau wengine wakiwemo matajiri wenye fedha kujitokeza kusaidia watoto yatima na wale wanaoishi kwenye mazingira magumu ili nao kuweza kuishi Mama ilivyobkwa watoto wengine. 

Awali katika risala ya taasisi Mwalimu wa Shule ya Msingi ya mchepuo wa kiingereza Muzdalifa iliyopo Mwakidila, Ibadi Saidi alisema wamekuwa wakitoa elimu kwa Yatima na watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu. 

Aidha ameipongeza Waterfall Charity UK kukubali kulipia karo watoto yatima wanaosoma shule mbalimbali hususani sekondari akisema,taasisi hiyo tayari imetumia zaidi ya Shilingi 70.5 milioni. 

Kwa mujibu wa Mwalimu,Said aamesema azma waliyokuwa nayo kwa sasa ni kupata mfadhili ili kuweza kujenga shule ya sekobdari huku akimshukuru Serikali kwa kujipambanua katika kuhakikisha usalama kwa wageni na ameiomba kuangalia uwezekano kuweka unafuu wa kodi ya ardhi kwenye maeneo yanayokusudiwa kumilikishwa Yatima. 

Mwanamkasi Nuru ni mlezi wa mtoto Nuru Musa (14),baada ya kukabidhiwa hati ya kumiliki nyumba alisema,anaamini maisha yake na kijana wake yanakwenda kubadilika akiondoka kwenye mazingira duni yaliyokuwa yakimkabili.

Amewasilisha shukrani zake kwa asasi ya Waterfall Charity UK na Masjid Muzdalifa kwa ushirikiano waliouonesha hadi kuhakikisha Yatima wanapata nyumba watakazo tumia katika maisha yao. 
Mwisho.



Pichani ni Katibu wa Masjid Muzdalifa,Twahir Twaha aliyemwakilisha Mkurugenzi wake Twaha Tawakal akitumia nafasi hiyo kwa kuwashukuru Waterfall Charity UK kwa ushirikiano waliouonesha hadi kufanikisha upatikanaji nyumba za watoto Yatima. 









Pichani ni Miongoni mwa nyumba zilizojengwa.

 

Friday 2 February 2024

RC TANGA,KINDAMBA ATUMIA UFUNGUZI WA MAADHIMINI YA WIKI YA SHERIA 2024 KUWAASA WANAOSAMBAZA ABARI ZA UZUSHI KWENYE MITANDAO ,,

Pichani wa pili kutoka mkono wa kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Tanga,Waziri Kindamba akiongoza matembezi ufunguzi maadhimisho ya Wiki ya sheria yaliyofanyika katika viwanja vya Tanga Urithi Jijini Tanga.

NA SOPHIA WAKATI,TANGA
MKUU wa Mkoa wa Tanga,Waziri Kindamba amesema,wanaoshiriki kusambaza habari za uzushi kwenye mitandao ya kijamii,hatua kali za kisheria hazitasita kuchukuliwa dhidi yao.

Kindamba aliyasema hayo alipokuwa mgeni rasmi kwenye ufunguzi maadhimisho ya Wiki ya sheria yanayofanyika katika viwanja vya Tanga Urithi Jijini Tanga.

Alielezea kusikitishwa kwake juu ya uzushi uliokuwa ukisambaa kupitia mitandao ya Kijamii kwamba mhanga mwingine wa ajali iliyohusisha msafara wa Naibu Waziri Mkuu Dk. Doto Biteko kudaiwa kufariki dunia.

Alisema, mhanga huyo amekuwa akiendelea kupatiwa matibabu katika hospitali ya rufaa Bombo na.kwamba ameanza kupata utambuzi licha ya awali kuwa katika hali mbaya.

"Hakuna faida yeyote kumsingizia mtu kifo sote njia ni hiyo hiyo hata uwe na fedha cheo iko siku na wewe utakwenda, jambo lililotendeka kwenye mitandao sikulipenda na kilichofanyika ni kosa la jinai"alisema Mkuu huyo wa mkoa Kindamba.

Kutokana na hali hiyo Kindamba alisema kwamba,hatua za kisheria zitachukuliwa kwa aliyeanzisha,aliyesambaza na hata kulikoleza jambo hilo ovu kwenye mitandao ya kijamii.

"Kiukweli tutawasaka na tutawachukulia hatua kali na hili ni kosa la mtandao,haina sababu kusingizia mwenzako kifo"alisema Kindamba kwa masikitiko makubwa. 

''Hivi majuzi Naibu Waziri Mkuu Dk. Doto Biteko aliyekuwa ziarani Mkoani Tanga gari walilopanda baadhi ya Waandishi wa habari na watumishi wa Tanga Uwasa waliokuwa kwenye msafara wake lilipata ajali''Alisema.

Ajali hiyo ilisababisha majeruhi ambao waliwahishwa Hospitali ya Bombo kwa ajili ya kupata matibabu ingawa kwa bahati mbaya mwandishi wa kituo cha Tanga TV Ally Haruna na Saidi Alawi dereva wa gari la Tanga Uwasa walifariki.

Haruna alizikwa kwenye makaburi ya Sharif Haidar Msamweni Jijini Tanga na Alawi alizikwa wilayani Pangani iliyopo mkoani Tanga ambapo kwenye ufunguzi Maadhimisho hayo Wiki ya sheria  Mahakama kuu kanda ya Tanga,Kindamba alitumia nafasi hiyo kwa kuwataka wadau kutumia muda mfupi kusimama kuwaombea Marehemu na wahanga wa ajali hiyo wapate kupona haraka kurejea kwenye majukumu yao.

Hata hivyo alisema serikali itaendelea kuwa nao bega kwa bega katika kuhakikisha wahanga wanapatiwa huduma stahiki ili atya zao kuweza kuimarika.
Mwisho.















 

Monday 29 January 2024

WANANCHI WILAYANI MUHEZA WANATARAJIWA KUNUFAIKA NA FEDHA ZA TOZO YA MAFUTA KUKARABATI BARABARA ZINAZOTUMIKA KWENYE MASHAMBA YA MACHUNGWA,,,



Pichani ni Meneja wa Wakala wa Barabara Vijijini TARURA Wilayani Muheza, Mhandisi John Frank Kwagilwa akiwa miongoni mwa barabara zilizopata fedha ya utekelezaji miradi kutoka serikalini.

NA SOPHIA WAKATI,MUHEZA
WANANCHI wa Halmashauri ya Wilaya ya Muheza Mkoani Tanga wanatarajia kunufaika na fedha za tozo ya mafuta baada ya kupata Milioni 950,220,000 ambazo zitatumika katika kufanya matengenezo kwenye miundombinu ya barabara zao.

 Taarifa hiyo imetolewa na Meneja wa Wakala wa Barabara Vijijini TARURA Wilayani Muheza,Mhandisi John Frank Kwagilwa alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari Ofisini kwake Wilayani humo.

Alisema kwamba kupitia fedha hizo barabara nyingi zitafanyiwa kazi zikiwemo zile zitakazounganisha vijiji vyenye Wakulima wa matunda hatua ambayo huenda ikasaidia kuleta tija kwenye sekta ya kilimo.

''Kuna fedha kutoka mfuko wa tozo kutoka Serikalini Shilingi 950,220,000 Milioni zitatumika kujenga barabara nyingi kwa kiwango cha changarawe''alisema Mhandisi huyo wa TARURA Muheza Kwagilwa.

AidA,Amezitaja barabara hizo zitakazofanyiwa matengenezo kuwa niza vijiji vya Kwakopwe - Mapinduzi 2.4 Km, Makuyuni - Kimwagamchuzi 2.8 Km, Makuyuni - Buhuri 4Km na Kwafungo - Kilongo 3.5 Kilomita na pia kunatarajiwa kujengwa vivuko.

Pia kuna barabara za Misozwe - Kwetango - Kambai - Msige 5 Km ,Mdote - Tanesco 0.6 Km, Genge - Mang'enya 2.0 Km, Muheza High school - Kivindo 1.66, Muheza Estate - Mkumbi 2.0 Km, Shidepha - Kididima 1.17 Km na Kwemuyu TRM - Ofisi ya Kata/Barabara ya Majengo 1.17.

Matengenezo mengine ni Box culvert,pipe culvert na matengenezo ya kawaida Mikwamba-Magila-Magoroto 4.0 Km, Amani-Kibaoni - Derema - Bulwa - Zirai -Bebere 5.0 Km,Mgeza - Kiwandamwenyeji 2.0 Km.

Kwa mujibu wa Mhandisi Kwagilwa alibainisha kwamba ujenzi wa barabara hizo ni matokeo ya kupokea mapendekezo kutoka kwenye vikao vya Kata ambavyo wenyeviti wake ni madiwani wanaopokea maoni ya Wananchi wialayani hapo.

 Katika utekelezaji huo wa mradi,Mhandisi Kwagilwa alisema kuwa, wananchi watapewa kipaumbele kwenye ajira za muda mara baada ya wakandarasi kutambulishwa lengo likiwa kuimarishwa kwa mahusiano ili kuleta ufanisi pindi mradi utakapokuwa ukitekelezwa.

Ujenzi wa mradi huo unatarajiwa kuanza mara baada ya michakato kukamilika hatua inayoendelea ni mchakato wa manunuzi na kuchukua nafasi yake na kazi tayari zimeshatangazwa.
Mwisho. 




 

Picha zote ni Meneja wa Wakala wa Barabara Vijijini TARURA Wilayani Muheza, Mhandisi John Frank Kwagilwa akiwa miongoni mwa barabara zilizopata fedha ya utekelezaji miradi kutoka serikalini.

WAFANYAKAZI WA SHIRIKA LA UMEME ZANZIBAR ZECO WAWEKA HISTORIA YA KUTEMBELEA VITUO VYA KUZALISHA UMEME 2024 TANGA,,



BAADA ya kutembelea Vituo vya Pangani  Hydro  Syestem Wafanyakazi wa Shirika la nishati ua Umeme Visiwani Zanzibar wamesema,ushirikiano na wenzao wa Tanesco utaimarika na hivyo kumudu kutatua mambo mengi kwa muda mfupi. 


Mkuu wa udhibiti mapato wa Shirika la Umeme Zanzibar Electricity Corporation (ZEC), Faina Idarus Faina amesema,katika ziara yao ya mafunzo mwaka 2024 tija itaonekana kwa Wafanyakazi wa pande zote mbili za Muungano.

Alisema,licha ya wao kushughulika na suala la Nishati hiyo ya Umeme kwa kuwahudumia Wananchi wa Visiwa vya Zanzibar lakini walikosa kujua namna ambavyo Nishati hiyo muhimu imekuwa ikizalilshwa.

Faina aliendelea kusema kwamba, ziara hiyo imekuwa darasa muhimu kwao, kwani waweza kujifunza mambo wasiyoyajua huku wakiimarisha uhusiano na wafanyakazi wenzao wa Tanzania bara.

Alisema,elimu waliyopata itawasaidia katika kuwaelimisha wateja wanaowahudumia pindi wanapolalamikia mambo ambayo hayakutokea kwa makusudi ila ni changamoto za kitaalam.

"Tumejua mengi ambayo hatukuwahi kuyajua,sie tumekuwa tukinunua umeme Tanzania bara kwa bulk na tunauza kwa wananchi"alisema Faina na kuongeza.

"Ziara yetu tumejifunza mengi,tumeimarisha uhusiano sasa tutatatua mambo mengi kwa wakati mmoja...pia tumepata elimu tutawaelimisha wateja wetu pindi wanapopiga yowe kukatika kwa umeme maana huwa sio kusudi"alisema Faina. 

Naye Kaimu Meneja wa Vituo vya kuzalisha Nishati ya Umeme Pangani Hydro Syestem, Kulwa Sosthenes alisema, wafanyakazi hao wa ZECO wametembelea vituo vya kuzalisha umeme wa nguvu ya maji New Pangani Force.

Sosthenes alisema kwamba,wageni hao wamejifunza jinsi umeme unavyozalishwa huku wakifahamiana na wenzao wa Tanzania bara hatua ambayo anaamini itaimarisha mahusiano na pia kuleta tija maeneo ya kazi.

Katika siku ya kwanza ya ziara yao Jijini Tanga,wakiwa wameambatana na Mbunge wa Jimbo la Amani Mkoa wa Mjini Magharibi Zanzibar, Abdul Yusuph Maalim, aliishauri Serikali kutenga fedha kwa ajili ya ziara za mafunzo kwa wafanyakazi wa taasisi. 

Mwisho. 



 Pichani ni mkuu wa kituo cha Hale Pangani  Hydro  Syestem,Kulwa Sosthenes akiwa ofisini kwake mara baada ya kuwapokea wafanyakazi wa shirika la umeme  ZECO Zanzibar.



Pichani ni kocha wa timu ya Soka ya Tanesco Tanga,Chausa Mganga akitangaza kuifua kikosi chake.

Kocha wa timu ya Soka ya Tanesco Tanga,Chausa Mganga ameahidi kuongeza makali mwaka 2024 kwenye kikosi chake hatua ambayo itawawezesha kupata ushindi mnono dhidi ya wapinzaji wake ambao watashuka dimbani kucheza michezo mbali mbali ikiwemo na ZECO kutoka Visiwani Zanzibar.


Chausa ametoa Matambo hayo Jiiini Tanga mara baada ya michezo ya Kirafiki dhidi ya Tanesco ya Zanzibar na matokeo ya mtanange huo uliopigwa Viwanja vya Popatlal yalikuwa mabao 2-2.

Baada ya michezo hiyo uliokuwa na upinzani mkali uliofanikiwa kuteka mashabiki wengi kutoka ndani ya Jiji la Tanga Viongozi wa timu zote mbili waliowapa fursa ya kutoa maoni yao.

Meneja wa Shirika la Umeme Tanesco Mkoani Tanga,Mathias Solongo aliyekuwepo kwenye mchezo huo alisema,licha ya kukubaliana na matokeo ya mchezo huo.lakini anaamini Vijana wake wangeweza kupata matokeo mazuri zaidi.

Alisema,vijana wake chini ya Mwalimu wao Chausa Mganga walionesha mchezo mzuri ikiwa ni ishara kwamba wameyaelewa mafunzo waliyopew na Mwalimu wao.

Hata hivyo,alisema kuwa pengine kilichowasababisha kupata sare hiyo ni kasoro ndogo ndogo ambazo sasa zitakwenda kufanyiwa kazi na kuwawezesha kupata ushindi kwa kila mchezo.

Ili waweze kufanya vyema kwenye michezo yao, Mhandisi Solongo alisema atahakikisha vijana hao wanapata maandalizi maazuri yatakayowawezesha kupata ushindi mchezoni.

"Timu yangu ni nzuri na niseme tu tutaendelea na.maandalizi ya kujiwinda kwa mchezo wa marudiano,nasi tutatafuta nafasi ya kuwafuata kule Zanzibar"alisema Solongo huku akiahidi kwenda kipata ushindi.

Naye Kiongozi wa timu ya Shirika la umeme Zanzibar Electricity Corporation (ZECO), alisema kwamba,hakuna ushindi wa kirahisi utakaopatikana kutoka kwa Vijana wake.

Alijinadi kuwa timu yake ni bora na Tanesco Tanga wajiandae kupogea kipigo pindi watakapokanyaga ardhi ya Visiwa vya Zanzibar. 

Pamoja na hayo pia alielezea kuridhishwa kwake na mapokezi mazuri waliyopata kutoka kwa wenyeji wa Tanesco Tanga akisema wamefarijika kwa ujarimu na ushirikiano waliopata.

Alisema kuwa,ziara hiyo ya michezo imewawezesha kujifunza mambo mbalimbali hatua ambayo itasaidia kuongeza ufanisi kwenye majukumu yao ya kazi. 

Mwisho.