TANZANIA imetajwa kuwa nchi ya pili katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara, kwa manunuzi na utumiaji wa simu za smartphone ikitanguliwa na Afrika Kusini.
Mkurugenzi wa kampuni ya bidhaa ya Puku, Meck Mbwana, alibainisha hayo jijini Dar es Salaam juzi wakati wa hafla ya uzinduzi wa kifaa hicho ambacho hutumika katika kuchaji simu za aina hiyo.
Alisema jambo hilo ndiyo sababu kubwa iliyowafanya kutambulisha Puku katika nchi hii kwa bara la Afrika, ambapo awali walilenga kuuza katika masoko ya Ulaya, hususani Marekani.
Alisema sababu nyingine ni kuweka uzalendo mbele, kwani asilimia 75 ya umiliki wa kampuni hiyo ni Watanzania huku asilimia 25 ikiwa ni Wamarekani.
Rais wa Puku Tanzania, Joseph Sikare, alisema pamoja na kuwepo kwa kifaa kama hicho kinachotengenezwa na makampuni mengine, wao wamekuja tofauti kwa kutengeneza kitu chenye ubora zaidi, mvuto kimuonekano na kinachodumu kwa muda mrefu.
Balozi wa Puku, Happiness Magese, aliwataka Watanzania kuwaunga mkono Puku, kwa maelezo kuwa wanatangaza utalii wa Tanzania duniani kupitia kifaa hicho ambacho jina lake ni aina ya mnyama wa swala anayepatikana Tanzania pekee.
No comments:
Post a Comment