Tuesday, 27 June 2017

OFISA UHAMIAJI MKOANI TANGA,,CRISPIN NGONYANI AKIELEZA JINSI WALIVYOFANIKIWA KUWANASA WAHAMIAJI HARAMU AMBAO WALIFICHWA KWENYE MASHAMBA YA WANANCHI NA KUHARIBU MAZAO,,,


 Pichani ni Mkuu wa Idara ya uhamiaji mkoani Tanga,Crispin Ngonyani akizungumza na waandishi wa habari hawapo pichani juu ya tukio lililotokea juzi saa 3:30 asubuhi baada ya taarifa kutoka kwa raia wema waliowafahamisha maafisa uhamiaji ambao walikuwa wakiwajibika kwenye mpaka wa Horohoro ambapo waliwafuatilia wahamiaji hao.

NA SOPHIA WAKATI,MKINGA
WAETHIOPIA 45 wamekamatwa wakiwa wamejificha kwenye mashamba ya Wananchi huko kijiji cha Horohoro wilayani Mkinga mkoani Tanga ambapo walikuwa wakimsubiri mtu aliyekuwa akiwatorosha wakati wa kifanya safari yao ya kuelekea Afrika kusini walikodai kuwa wanakwenda kutafuta maisha.

Mkuu wa Idara ya uhamiaji mkoani Tanga,Crispin Ngonyani amesema kuwa tukio hilo limetokea saa 3:30 asubuhi baada ya taarifa kutoka kwa raia wema waliowafahamisha maafisa uhamiaji ambao walikuwa wakiwajibika kwenye mpaka wa Horohoro ambapo waliwafuatilia wahamiaji hao.

Alisema,wahamiaji hao baada ya kukamatwa walisema walikuwa kwenye mashamba hayo wakiwa wanamsubiri aliyekuwa akiwasafirisha ambaye alikuwa akikagua njia ili kuweza kupita pasipo kutiwa nguvuni ambapo taarifa zinaeleza kuwa kwenye maeneo hayo waliharibu mazao ya wananchi.

Mkuu huyo wa Idara ya uhamiaji alisema kwamba raia hao wa Ethiopia kwenye mashamba hayo walikutwa wakivuna mahindi mabichi na kuyala mazingira ambayo huenda yakawa yamesababishwa na njaa ambayo ilikuwa ikiwakumbua ndipo wananchi kuwafahamisha askari ambao waliwakamata.

Aidha mkuu huyo wa uhamiaji alisema,vitendo vya uhamiaji usiozingatia sheria limekuwa likiongezeka ambapo jitihada zitaendelea kufanywa kuwapatia elimu wananchi ili kusaidiana na serikali kupiga vita matukio ya aina hiyo ambayo kwa upande mwingine yanaweza kuchangia kuhatarisha usalama.

Kwa mujibu wa afisa huyo,Ngonyani alibainisha imekuwa ni kawaida kwa Waethiopia hao kudai wanapita kama njia kwenda Afrika kusini kwa ajili ya kutafuta maisha ambapo ameishauri jamii kuendelea kushirikiana kwa karibu na uhamiaji lengo likiwa kuondosha kabisa vitendo hivyo visivyozingatia misingi ya sheria.

Hata hivyo,pamoja na kiongozi huyo wa uhamiaji alisema kwamba wapo baadhi ya watu ambao wanajihusisha na kuishi nchini kinyume na taratibu za sheria baada ya vibali vyao kuisha muda ambapo amewasihi watu wa namna hiyo kufuata taratibu kabla hawajabainika na kuchukuliwa hatua za kisheria ikiwemo ile ya kulipa faini na kufungwa jela.

Vilevile alisema kwamba katika kuhakikisha kuwa wanadhibiti vitendo hivyo idara ya uhamiaji mkoani Tanga imeweka Vizuizi barabarani maeneo ambayo upekuzi hufanyika lengo likiwa kuwabaini wahamiaji hao wasiozingatia sheria huku akiwasihi wale ambao vibali vyao vimeisha kufuata utaratibu stahiki.

Hata hivyo,pia alitumia nafasi hiyo kwa kuwataka wananchi wanaoshi pembezoni mwa mpaka wa nchi jirani Kenya kuendelea kuwaamini na kutoa ushirikiano lengo likiwa kudhibiti vitendo vya uhamiaji mkoani hapo.
Mwisho.

No comments:

Post a Comment