Sunday 22 October 2017

CCM MKOANI TANGA YASISITIZA VIONGOZI NA WANACHAMA KULETA MABADILIKO NDANI YA CHAMA,,,

Pichani ni katibu wa CCM mkoa wa Tanga,Allan Kingazi akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake akisisitiza viongozi na wananchama kuleta mabadiliko ndani ya CCM.

NA SOPHIA WAKATI, TANGA
KATIBU wa chama cha mapinduzi CCM mkoani Tanga,Allan Kingazi amesema uchaguzi kujaza nafasi mbalimbali za uongozi umekwisha akiwataka wanachama kushirikiana na viongozi wao kuiletea mabadiliko CCM. 

Kingazi ameyasema hayo juzi akisema baada ya uchaguzi ndani ya chama chao kumalizika kinachohitajika ni mabadiliko huku akiwasihi viongozi kushirikiana na wanachama kuimarisha ngome za chama cha mapinduzi CCM. 

"Tunashukuru uchaguzi umemalizika vizuri kilichobaki ni kujenga Chama, baada ya wanachama kuwaweka viongozi madarakani washirikiane nao kuimarisha ngome ili kukiletea chama mabadiliko makubwa"alisema Kingazi. 

Wakati,Kingazi akiyasema hayo,mwenyekiti wa CCM wilayani Tanga,Meja mstaafu Hamisi Mkoba amewataka viongozi wenzake kuanzia ngazi ya matawi na mashina kuhakikisha kipaumbele chao kuwa kurejesha hadhi ya CCM jijini hapo. 

Alisema, viongozi waliochaguliwa wanapaswa kutambua kuwa chama chao kimejijengea heshima kubwa miongoni mwa jamii hivyo wana kila sababu kukitukikia kwa uadilifu ili kuendelea kudumisha heshima iliyokuwa nayo CCM. 

Pia,amewataka wana CCM kuwa na uchungu na chama chao katika kukitetea huku akiwataka kuunganisha nguvu zao kurejesha kata 13 zilizokwenda upinzani. 

"Kiukweli nitoe shukrani kwa kuchaguliwa sasa naomba ushirikiano twendeni kwenye maeneo yetu kupigania maslahi ya CCM, kila mmoja wetu awe na uchungu na CCM "alisema Meja mstaafu Mkoba. 

Mwenyekiti huyo wa CCM wilayani Tanga,alisema kwamba kulingana na heshima kubwa ya chama hivyo miongoni mwa jamii kuna uwezekano mkubwa kurejesha kata zilizopotea akisisitiza uwepo mshikamano madhubuti. 

Mkoba amesema, kupitia mshikamano wao ana matumaini makubwa kwamba CCM itaendelea kuheshimika miongoni mwa jamii huku chama hicho kikiendelea kupata ridhaa ya kuwatumikia watanzania.
Mwisho.



No comments:

Post a Comment