Sunday 15 October 2017

KATIBU TAWALA WILAYA YA KOROGWE AKIFUNGUA MRADI WA MAJI KATA LUTINDI,,,



 Pichani ni katibu tawala wa wilaya ya Korogwe,Rehema Said Bwasi aliyemwakilisha mkuu wa wilaya hiyo,Mhandisi Robert Gabriel. akifungua mradi wa maji juzi kata ya Lutindi wilayani hapo.



NA SOPHIA WAKATI,KOROGWE
WANANCHI wa vitongoji vya Nazareth juu na Gombelo huko kata ya Lutindi wilayani Korogwe wameondokana na kero ya kutembea umbali mrefu kusaka maji baada ya mradi uliogharimu kiasi cha sh 7 milioni kukamilika.

Mradi huo ambao umezinduliwa juzi na katibu tawala wa wilaya ya Korogwe,Rehema Bwasi aliyemwakilisha mkuu wa wilaya hiyo,Mhandisi Robert Gabriel. 

Baada ya kuzindua mradi huo wa jamii uliojengwa kwa ufadhili wa mtawala wa hospitali ya magojwa ya akili kwa kushirikiana na wananchi katibu tawala alihimiza utunzaji mazingira na misitu katika vyanzo vya maji. 

Alisema, ili mradi huo kuwa endelevu kwa maslahi ya vizazi vya sasa na vijavyo wananchi hawana budi wanapaswa kuepuka vitendo vya uharibifu wa mazingira kwa kukata miti ovyo ama kuchoma misitu. 

Alitumia wasaa huo kumpongeza mtawala wa hospitali hiyo ya Lutindi,Tim Hammerbacher kwa hatua yake kusaidia huduma za jamii kuondoa kero hiyo ya maji. 

Awali akisoma taarifa ya mradi huo kwa mgeni rasmi Afisa mtendaji wa kijiji cha Lutindi,Gerdath Nyangasa alisema mfadhili huyo amechangia sh 5 milioni kwa ajili ya ununuzi wa vifaa na kulipia ufundi. 

Aidha afisa huyo,alisema kwamba wananchi wakiwa wamechangia nguvu kazi ikiwemo kuchimba mitaro ambayo ni sawa na sh 2 milioni hivyo kufanya  jumla ya sh 7 milioni za kitanzani kuwa gharama halisi ya mradi. 

Vilevile afisa huyo alibainisha kwamba familia ya mzee Elikana Madeni imetoa eneo lao kwa ajili ya kufanikisha ujenzi wa tenki la kuhifadhia maji lenye uwezo wa kubeba lita 20,000.

Nae diwani wa kata ya Lutindi,Nicolas Shemsanga alisema, ingawa mradi huo ulilengwa kwa vitongoji viwili lakini una uwezo wa kuhudumia vitongoji zaidi ya hivyo. 

Pia,alitumia nafasi hiyo kumpongeza mfadhili ambaye ni mtawala wa hospitali ya magonjwa ya akili Lutindi, Tim Hammerbacher akimweleza kuwa amekuwa na msaada mkubwa kujitolea kwenye huduma za jamii akitolea mfano barabara. 
Mwisho.

 Pichani ni katibu tawala wa wilaya ya Korogwe,Rehema Said Bwasi aliyemwakilisha mkuu wa wilaya hiyo,Mhandisi Robert Gabriel. juzi mara baada ya kufungua mradi wa maji kata ya Lutindi wilayani hapo akimtwika mkazi wa Gombero ndoo ya maji..

No comments:

Post a Comment