NA SOPHIA WAKATI,TANGA
KAMANDA wa Polisi
Mkoani Tanga, Safia Jongo, amekemea vikali ukatili wa kijinsia na kisaikolojia, amewasihi Watanzania kuacha
vitendo hivyo ambavyo vimekuwa vikileta sura mbaya kwa Taifa.
Kamanda Jongo ametoa ombi hilo juzi wakati alipotembelea Shule ya watoto wenye
ulemavu Pongwe,kituo cha watoto yatima na gereza la Maweni vilivyopo
Halmashauri ya Jiji la Tanga.
Katika ziara yake hiyo, Jongo aliambatana na askari polisi wanawake 'Tanzania
Police Women Network' dawati la jinsia,ustawi wa jamii na taasisi nyingine
ambazo ni sehemu ya wadau wa haki za watoto.
Alisema kuwa ziara hiyo imekuja katika siku 16 za kupinga ukatili dhidi ya jinsia na watoto ambayo
huadhimishwa kimataifa na Tanzania kwa ujumla.
Alisema lengo kubwa la siku hizo ni kupambana na ukatili wa jinsia na watoto na kwamba mbali na
shughuli ya uelimishaji jamii wameona umuhimu kuwatembelea watoto wenye ulemavu
Pongwe.
Watoto hao waliotembelewa ni wale wenye uoni hafifu na ulemavu wa ngozi wakiwa
miongoni mwa makundi yaliyoathirika sana na ukatili hata kufikia hatua ya kutengwa na kufichwa majumbani
wakionekana kuwa
mkosi.
Kutokana na hali hiyo,Kamanda Jongo amewaasa watanzania kuacha vitendo
vya ukatili wa aina zote kwa
madai kuwa vinachafua nchi na amehimiza mshikamano kutokomeza suala hilo.
"Siku 16 huadhimishwa kimataifa na mkoa tukaona tuungane na wenzetu
kimataifa na Tanzania katika kupambana na ukatili wa jinsia na
watoto"alisema.
Johgoakiwa katika ziara hiyo amewaeleza watoto hao wa shule ya walemavu Pongwe
kuwa wanapaswa kuona kwamba wanazo nafasi za kuwa viongozi kwenye Taifa hili
huku akiwasihi kuongeza bidii kwenye masomo yao.
"Kikubwa ni kuwa na bidii kwenye masomo mnaweza kuwa Rais,mawaziri na hata
askari polisi,ni lazima muwe na ndoto za kuwa na maisha bora ya baadae na kuwa
na familia"alisema kamanda Jongo.
Amelieleza kundi hilo la walemavu kwamba linategemewa na serikali huku akiisihi
jamii kuwaangalia kwa uoni maalum watoto wenye ulemavu mbalimbali.
Aidha aliwaasa wazazi kutokukata tamaa juu ya watoto wenye ulemavu akiwasihi
kuwapeleka shule ili kupata haki yao kwani kinyume chake ni
kitendo cha ukatili.
Amesema shule ya msingi Pongwe yenye watoto wenye ulemavu inazo nafasi kupokea
watoto hao ambapo jamii inapaswa kuitumia huku akiongeza kuwa suala la
mifarakano ya wazazi ni sehemu ya ukatili ambao mwisho wake hupatikana watoto wahalifu.
Katika ziara hiyo ya siku 16 kupinga ukatili jeshi la polisi na wadau wake wametembelea maeneo
mbalimbali sanjari na kutoa vifaa mchanganyiko vilivyogharimu Tsh 4 million.
Diwani wa Kata ya Pongwe,Mbaraka Saad amelipongeza jeshi la polisi,akisema ujio
wao umeleta faraja kwa watoto hao wenye ulemavu akiwasihi wadau wengine kuiga
mfano huo.
Naye Afisa maendeleo jamii wa halmashauri ya Jiji la Tanga,Bertha Dama alisema
lengo la kuwa na siku 16 za ukatili wa kijinsia ni kutoa elimu ya ufahamu kwa jamii ili
kuelewa madhara na athari zinazotokana na ukatili wa kijinsia.
Alisema Jiji la Tanga linakabiliwa na changamoto ya ukatili wa kijinsia kuanzia ngazi ya familia
ambapo wazazi wameacha wajibu wa kuwalinda na kulinda usalama wa watoto
Mwisho.
No comments:
Post a Comment