Monday, 13 February 2023

POLISI TANGA ILIVYOFANIKIWA KUWAKAMATA VIJANA 14 KWA TUHUMA ZA KUHUSIKA NA WIZI AJALI YA COASTA NA FUSO WILAYANI KOROGWE,,,



Pichani ni Kamanda wa jeshi la polisi mkoani Tanga,Henry Mwaibambe akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake sakata la kuwakamata vijana 14 kwa tuhuma za kuhusika na vitendo vya wizi ajali ya iliyohusisha gari aina ya Coasta na Fuso wilayani Korogwe na kusababisha vifo 21 na majeruhi akiwa na msaidizi wake kushoto.

NA SOPHIA WAKATI, TANGA
WATU 14 wanashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoani Tanga wakihusishwa na vitendo vya Wizi wa kuwaibia Wahanga wa ajali iliyohusisha magari mawili yaliyogongana uso kwa uso eneo la Magila Gereza Wilayani Korogwe.

Kamanda wa Polisi Mkoani Tanga,Henry Mwaibambe akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake juzi alisema kwamba baada ya kutokea kwa ajali hiyo iliyohusisha gari aina ya Coasta na Fuso kupata taarifa kutoka kwa baadhi ya ndugu kuna vijana wamevamia na kupora vitu.


Alisema kuwa baada ya kupata taarifa hiyo walijipanga na kuanza kufanya msako katika vijiji vya jirani Gereza,Kwasunga na Msambiazi ili kuwabaini wahalifu na kunusuru mali.

"Kwenye operesheni hiyo tulifanikiwa kuwakamata watu 14 wakishukiwa kuwaibia vitu mbalimbali ikiwemo vyakula majeruhi na marehemu wa ajali hiyo iliyohusisha gari aina ya Coastar na Fusso''alisema Kamanda Mwaibambe.

Kwa mujibu wa Kamanda huyo wa jeshi la Polisi,alisema  miongoni mwa waliokamatwa, katika mahojiano wapo waliokiri kutenda vitendo hivyo vya wizi na kwamba uchunguzi bado unaendelea.

Alisema kwamba, katika upelelezi wao, polisi wanashirikiana na ndugu walioshuhudia ajali hiyo ambao walikuwa kwenye gari lililokuwa nyuma ya  Coastar iliyobeba Maiti ikisafirisha ambayo iligongana na Fusso.

Inaelezwa kuwa, baada ya ajali hiyo kutokea baadhi ya watu badala ya kutoa msaada walishiriki kuwaibia wale waliokumbwa na kadhia hiyo na kutoweka.

Hata hivyo mara baada ya taarifa za tukio hilo kulifikia Jeshi la Polisi ndipo uchunguzi ukaanza na hivyo kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao.

"Kiukweli katika mahojiano wapo waliokiri kuhusika kuiba vitu mbalimbali kwenye ajali hiyo na kwenda kuonyesha"alisema Kamanda Mwaibambe na kusisitiza kuwa upelelezi unaendelea ili kuwabaini wote waliohusika.

Akizungumzia zaidi ameeleza kwamba, majeruhi wote waliokuwa wakitibiwa katika hospitali ya Bombo wameruhusiwa huku akiwa amebaki mmoja tu ambaye amevunjika miguu yote miwili na anendelea kupatiwa matibabu.

Aidha,amemtaja majeruhi huyo kuwa ni Florence Mrema (42) ambaye ni ndugu wa marehemu wa ajali hiyo iliyoua zaidi ya watu 17 wilayani Korogwe mkoani Tanga na baada ya upelelezi kukamili watapandishwa mahakamani.
Mwisho.


 

No comments:

Post a Comment