Monday, 26 October 2026

SERIKALI IMEANZA KUTEKELEZA MPANGO WA BIMA YA AFYA KWA WOTE

Picha ni Meneja wa Bima ya afa mkoa wa Tanga,Evans Nyangasa akiwasilisha taarifa yake mpango uliopo kuhahakikisha walengwa wanapata kado za bima kwa wote.



 NA SOPHIA WAKATI,HANDENI

SERIKALI imeanza kutekeleza mpango wa Bima ya Afya kwa Wote, huku Mkoa wa Tanga ukilenga kusajili kaya 27,233 zenye jumla ya wanufaika 59,552 katika awamu ya pili ya mpango huo.


Katika awamu hiyo, kaya zisizo na uwezo wa kifedha pamoja na kaya zenye uwezo zitasajiliwa kwa wakati mmoja ili kuwawezesha wananchi kupata huduma za matibabu kwa uhakika na kwa wakati wanapozihitaji.


Katika taarifa yake kwenye uzinduzi wa zoezi la usajili uliofanyika Mkata Mashariki, wilayani Handeni, Meneja wa Bima ya afya (NHIF) Mkoa wa Tanga, Evans Nyangasa amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kujiunga na mpango huo.


Alisema, mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Mkoa wa Tanga katika awamu ya kwanza ya mpango wa uhakiki na uandikishaji wa kaya zisizo na uwezo, jumla ya kaya 10,189 ziliandikishwa na kupewa kadi za matibabu.


Alisema kwamba,idadi hiyo ni sawa na asilimia 75% ya kaya 13,100 ambazo zilikuwa zimelengwa kutoka katika halmashauri zote za Mkoa huo wa Tanga.


Alieleza kuwa zoezi hilo lilifanyika kuanzia Februari 3 hadi Septemba 30, 2026, na kwamba katika awamu ya pili mkoa unalenga kusajili kaya 27,233 zenye wanufaika 59,552.


Alisema utekelezaji wa mpango huo utahusisha uandikishaji wa wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (TASAF), kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, halmashauri, waratibu wa TASAF, Wizara ya Afya, waratibu wa bima ya afya na wahudumu wa afya ngazi ya jamii.


Kwa mujibu wa meneja huyo, amesema tayari NHIF imepata mdau wa maendeleo, GIZ Tanzania, aliye tayari kufadhili zoezi hilo la awamu ya pili, likianzia Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi.


Alisema zoezi hilo linatarajiwa kuanza Novemba 2 mwaka huu.

Meneja huyo aliongeza kuwa NHIF itaendelea kushirikiana na wadau katika usajili na utoaji wa kadi za matibabu, pamoja na kuhakikisha taarifa za walengwa zinatambuliwa na kuthibitishwa ili wanaostahili wanufaike na huduma hizo.


Alisema mfuko huo unaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa bima ya afya, taratibu za kupata kadi na namna ya kuzitumia katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya vilivyosajiliwa ndani na nje ya mkoa wa Tanga.


Aliwaomba viongozi wa mkoa, halmashauri, watendaji wa mitaa na viongozi wa ngazi nyingine kushiriki katika uhamasishaji ili kuhakikisha kuwa walengwa wanapata taarifa na kujitokeza kwa ajili ya kufanya uhakiki na usajili.


Aidha, alizitaka halmashauri kuhakikisha kwamba taarifa za walengwa zinathibitishwa kwa wakati, huku vituo vya kutolea huduma za afya vikiimarisha maandalizi ya kutoa huduma bora kwa wanufaika wa mpango huo.


Kaimu Katibu tawala wa Mkoa wa Tanga Amina Said alisema bima ya afya ina umuhimu mkubwa katika kupunguza mzigo wa gharama za matibabu kwa familia na Serikali, huku ikiimarisha usawa katika upatikanaji wa huduma za afya.


“Afya bora huwawezesha wananchi kushiriki katika shughuli za uzalishaji na hivyo kukuza uchumi. Bima ya afya inapunguza mzigo wa matibabu kwa familia na hata Serikali,” alisema Amina.


Aliongeza kusema kuwa bima hiyo inatoa fursa ya kupata huduma za afya kwa wakati bila kujali uwezo wa kifedha wa wananchi, sambamba na kuongeza usawa katika upatikanaji wa huduma, ikiwemo za kibingwa katika ngazi mbalimbali za vituo vya afya.


Alisema Serikali imeanza rasmi kutekeleza Sheria ya Bima ya Afya kwa wote Februari 2026, ikiwalenga pia wananchi wa makundi maalumu wasio na uwezo, wakiwemo wazee, watoto, wajawazito na wenye ulemavu.


Alisema Serikali imetoa fedha kwa ajili ya kugharamia makundi hayo ili kuhakikisha yanapata huduma za matibabu na ahueni sawa na makundi mengine yenye kipato.


Aidha, aliwataka wananchi kuchangamkia fursa ya kujiunga na bima hiyo kwa kuchangia Sh 150,000 kwa kila kaya yenye watu wasiozidi sita akisisitiza kuwa afya ni msingi wa maendeleo ya mtu mmoja mmoja, familia na taifa.


Akizungumzia tahadhari za kiafya na mazingira, Amina aliwataka wananchi kuzingatia usafi wa mazingira kutokana na taarifa za uwezekano wa kutokea kwa mvua za El Nino, aliwashauri wanaoishi kwenye maeneo ya mabondeni kuhama mapema ili kujikinga na athari zinazoweza kujitokeza.


Alisema hatua hizo ni muhimu.








No comments:

Post a Comment