Wednesday, 7 September 2022

HAFLA YA UZINDUZI WA MATAWI MANNE YA MFUKO WA SEIF MICROFINANCE FUND ILIKUWA HIVI,,,JIJINI TANGA,

Pichani katikati ni Mkuu wa Mkoa wa Tanga,Omari Mgumba akizitaka Halmashauri zote za mkoa huo kujifunza kutoka Mfuko wa fedha wa Self Microfinance Fund kuhusu namna bora ya kutoa Mikopo kwa Wananchi hatua ambayo pia itasaidia upatikanaji marejesho kufanyika kwa ufanisi.

Pichani ambaye ameshika kipaza sauti ni Mkuu wa Mkoa wa Tanga,Omari Mgumba akiwa na viongozi mbalimbali kwenye hafla ya Uzinduzi wa matawi manne ya Mfuko huo wa Self Microfinance Fund ambayo ni tawi la Tanga, Morogoro, Iringa na Mtwara, shughuli ambayo imefanyika Jijini Tanga.


 NA SOPHIA WAKATI,TANGA

MKUU wa Mkoa wa Tanga,Omari Mgumba amezitaka Halmashauri zote za mkoa huo kujifunza kutoka Mfuko wa fedha wa Self Microfinance Fund kuhusu namna bora ya kutoa Mikopo kwa Wananchi hatua ambayo pia inasaidia marejesho kufanyika kwa ufanisi.

Mgumba alitoa wito huo juzi kwenye hafla ya Uzinduzi wa matawi manne ya Mfuko huo wa Self Microfinance Fund ambayo ni tawi la Tanga, Morogoro, Iringa na Mtwara, shughuli ambayo imefanyika Jijini Tanga.

Alifikia hatua hiyo, baada ya kuridhishwa na taarifa ya mfuko wa Self Microfinance Fund iliyoeleza kuwa urejeshwaji wa mikopo umekuwa wa kuridhisha ambapo ni zaidi ya asilimia 83 inayorejeshwa kwa wakati.

"Nitoe wito kwa halmashauri zote 11 za mkoa wa Tanga kuja kujifunza mbinu na mikakati kwa Self Microfinance Fund namna walivyofanikiwa kurejesha mikopo kufikia 80%"alisema Mgumba.

Mgumba alisema kwamba,asilimia 10% kutoka kwenye mapato ya ndani ya halmashauri zinapaswa kurejeshwa kwa wakati ili kuwafikia watanzania walio wengi na kumudu kuinua uchumi wao.

Hata hivyo alisema,hali ya urejeshaji mikopo kwa wanawake ni yenye kuridhisha tofauti na vijana ambao wanapaswa kuwaiga wanawake ili kuweza kukopesheka.

Alitumia nafasi hiyo kuipongeza taasisi hiyo ya umma (Self 
 Microfinance  Fund) kwa kutoa mikopo yenye riba nafuu kwa kuweza kukuza mtaji kutoka Bilioni 57 mwaka 2016 hadi 59.8 Bilioni juni 2022.

Awali,Mkurugenzi mtendaji wa Self Microfinance Fund, Mudith Cheyo akiwasilisha taarifa yake alisema,uamuzi wa kufungua matawi Tanga,Morogoro,Iringa na Mtwara ni sehemu ya mkakati wao lengo kuunga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya sita katika kuboresha maisha ya Watanzania.

Cheyo alisema,tangu mwanzoni mwa mwaka huu waliweka mkakati huo wa kufungua matawi mapya ili kurahisisha utoaji wa huduma zaidi za mikopo kwa riba nafuu huku wakiahidi kuongeza wigo.

Alisema,matawi hayo mapya yatawarahisishia kazi wananchi waliokuwa wakilazimika kusafiri kutoka mkoa mmoja kwenda mwingine kwa ajili ya kufuata huduma za kifedha katika taasisi hiyo.

Cheyo alibainisha kuwa, mikopo wanayotoa ni ile ya wafanyakazi wadogo, kati na wakubwa ambapo pia wamekuwa wakitoa mikopo kwa wafanyabiashara
kwa utaratibu uliowekwa baada ya kutengewa maeneo ya kuendeshea shughuli zao.

Kwa upande mwingine,Cheyo alisema, Self Microfinance Foundation imetoa vitanda na magodoro 80 kwa Chuo cha Walemavu Yombo Dar es salaam, fenicha ambazo zimegharimu Shilingi 29,390,600.00 ili kusaidia jamii.
Mwisho.

No comments:

Post a Comment