Tuesday, 8 November 2022

HTM WILAYANI KORONGWE IMEJIPANGA KUONDOA CHANGAMOTO YA UKOSEFU WA MAJI MAENEO MBALIMBALI IKIWEMO KWA WANANCHI WA HANDENI,,


 Pichani ni Mkurugenzi Mtendaji wa HTM wilayani Korogwe,Mhandisi Yohana Mgaza ofisini kwake akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) mpango mkakati uliopo kuondoa changamoto ya ukosefu wa maji safi na salama kwa wananchi ikiwemo wilayani Handeni.


NA SOPHIA WAKATI,KOROGWE
MAMLAKA ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Handeni Trunk Main (HTM), ina mpango mkakati wa kufanya Ukarabati mkubwa kwenye Miundombinu yake iliyojengwa mwaka 1974 ili kuondoa uchakavu wa miundombinu.

Hata hivyo,imesema lengo likiwa ni kurahisisha upatikanaji wa huduma ya Maji safi na salama kwa Wananchi kuwaondolea usumbufu wa kutembea umbali mrefu kufuata huduma hiyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa HTM wilayani Korogwe,Mhandisi Yohana Mgaza, aliyasema hayo juzi ofisini kwake kwamba lengo kuondoa changamoto ya ukosefu wa maji safi na salama kwa wananchi.

Mhandisi Mgaza alikuwa akijibu Swali la waandishi wa habari aliyetaka kujua jinsi HTM ilivyojipanga katika kutatua changamoto ya Maji kwa Kambi ya Jeshi la Kujenga Taifa JKT Mgambo  iliyopo Kabuku Wilayani Handeni.

Akitoa ufafanuzi juu ya kero ya ukosefu wa maji inayotajwa kuwepo kambini hapo,alisema, kuna wakati husababishwa na ukame na suala la upungufu wa nishati ya umeme.

Aidha alisema,pia mamlaka imeanza kuchukua hatua madhubuti kuchimba visima virefu vitakavyotumika vipindi vya dharura huku mradi mkubwa wa Miji 28 utakaogusa mradi wa HTM ukiaminika kuwa muarobaini wa kero ya
maji kwenye maeneo mbalimbali ya wilaya ya Handeni na wilaya za Pangani,Muheza na Pangani.

Kuhusu mradi huo wa Miji 28 ni kutokana na fedha za mkopo nafuu kutoka Serikali ya India,alisema kuwa pindi ukikamilika utakuwa mkombozi wa wananchi wilayani Handeni na hata kambi ya JKT Mgambo.

Alisema, mkandarasi ameshapatikana ambapo kwa sasa anafanya usanifu utakaodumu kwa miezi mitatu ikitarajiwa kuwa ifikapo mwezi disemba ataanza kutekeleza kazi ya ujenzi.

Aidha,alibainisha kueleza kwamba baada ya kazi kuanza,matarajio ni miji jirani kuanza kupata maji katika kipindi cha miezi sita na utakapofika mwaka mmoja eneo kubwa zaidi litaweza kupata huduma stahiki.

Mhandisi Mgaya,mradi huo wa HTM kwa sasa uwezo wake ni kuzalisha lita milioni nne za maji na baada ya ukarabati kufanyika uzalishaji utaongezeka hadi kufikia lita 52 milioni.

Kutokana na hali hiyo kutakuwa na maji yatakayoweza kuhudumia watu wote kwenye wilaya za Handeni vijijini, Pangani, Korogwe na Muheza mradi ambao unatarajiwa kugharimu sh 200 bilioni.
Mwisho.


No comments:

Post a Comment