Wednesday, 1 March 2023

WANANCHI WA MTAA WA SWAHILI MAGAONI WAMEISHUKURU TASAF KUIBUA MIRADI MIWILI MUHIMU,,,,

Pichani ni miongoni mwa wanufaika wa mpango wa TASAF mtaa wa Swahili kata ya Magaoni,Mery Kaji amesema, anaishukuru serikal kwa kufanikiwa kuibua miradi miwili wa usafi wa mfereji na kufungua barabara kwani tangu kujengwa kwa mfereji huo haujawahi kusafishwa na kusababisha mafuriko.


NA SOPHIA WAKATI,TANGA

WANANCHI wa Kata ya Magaoni iliyopo Halmashauri ya Jiji la Tanga, wamefanikiwa kujikwamua kiuchumi baada ya wengi wao kuhamasika kuingia kwenye taratibu za ajira za muda kupitia mpango wa TASAF kunusuru Kaya
Masikini.

Afisa Mtendaji mtaa wa Swahili uliopo kata ya Magaoni, Maua Haniu alisema kupitia ajira za muda wananchi wameibua mradi wa kusafisha mfereji mama ili kuondoa kero ya mafuriko kipindi cha mvua.

Alisema kwamba kupitia mpango huo wa TASAF Wananchi wa mtaa wa Swahili wamepata miradi miwili inayotoa ajira za muda kwa jamii husika ambapo changamoto zilizowakabili sasa zinatatuliwa kirahisi.

Anaitaja miradi hiyo kuwa ni kusafisha Mfereji na kurekebisha barabara ili kuweza kuzifungua na kurahisisha magari kuweza kuingia.

 Afisa huyo,Maua alibainisha kueleza kwamba kukamilika kwa mradi wa barabara utasaidia wananchi kupata huduma kwa karibu na usafishaji mfereji ambao utaondosha changamoto ya mafuriko kwenye makazi ya wanufaika walengwa 37.

Kwa upande wake,miongoni mwa wanufaika wa mpango wa TASAF kata ya Magaoni,Mery Kaji ambaye ni mkazi wa mtaa wa Swahili amesema, anaishukuru kwa miradi hiyo kwani tangu kujengwa kwa mfereji huo haujawahi kusafishwa.

''Tulipopata fursa ya kupendekeza miradi,tulichagua mradi wa mfereji na barabara kutokana na kero zinazojitokeza''Alisema mkazi huyo wa mtaa wa Swahili Mery huku akiishukuru TASAF.

Alisema kuwa miradi hiyo ni muhimu sana kutokana na maafa ambayo yamejitokeza kipindi cha nyuma yanapotokea mafuriko kipindi cha mvua.

Akizungumzia zaidi mradi wa ajira za muda unaotekelezwa na TASAF, Mery alisema,kufunguka kwa barabara itasaidia wajasiliamali kupitisha bidhaa kusafirisha mpaka majumbani.

Alisema, kupita mradi huo wananchi wataondokana na kero ya mafuriko ya mara kwa mara iliyowakumba katika makazi yao nyakati mvua ziliponyesha.

Alisema, kwa mambo makubwa yanayofanywa na Serikali ya awamu ya sita iko haja ya kumsaidia kwa vitendo Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.
Mwisho.





 

No comments:

Post a Comment