Tuesday, 28 March 2023

ZIARA YA KATIBU WA CCM MKOA WA TANGA WILAYANI MUHEZA,KUJIONEA CHANGAMOTO YA MAJI ILIKUWA HIVI,,,,


Picha mkono wa kushoto ni Katibu wa CCM mkoa wa Tanga,Suleiman Mzee Suleiman katika ziara yake ya kutembelea vyanzo vya maji Muheza akipata taarifa kutoka kwa Meneja wa Tanga Uwasa wilayani Muheza,Ramadhan Nyambuka wa pili akielezea mitadi ya maji mbalimbali ambayo imepata pesa kutoka serikalin wa tatu ni mfuatiliaji wa miradi wa Tanga Uwasa,Rashid Shaban na kulia ni katibu wa CCM Wilaya ya Muheza. 

NA SOPHIA WAKATI,MUHEZA
Chama Cha Mapinduzi CCM Mkoa wa Tanga kimebaini kwamba, upungufu wa Maji Wilayani Muheza unachangiwa na baadhi ya Watu kushiriki vitendo vya Uharibifu wa mazingira kwenye vyanzo vya maji hususani Mto Mkurumuzi.

Kutokana na hali hiyo,Katibu wa CCM Mkoani Tanga, Suleiman Mzee Suleiman ameielekeza Serikali kuhakikisha kuwa vyanzo vya maji vinadhibitiwa ikiwemo wananchi kupatiwa elimu.

"Wote wanaoishi kwenye vyanzo vya maji lazima Serikali ijipange na wataalam wake kuanza kufanya ziara kukagua vyanzo vyote,yanayohitaji kuwa reserved  yadhibitiwe kwa namna yeyote itakavyoweza kujipanga" alisema Katibu huyo wa CCM Mkoa wa Tanga Suleiman.

Akizungumzia zaidi kuhusu changamoto ya maji wilayani Muheza Katibu wa CCM Mkoa wa Tanga,Suleiman Mzee Suleiman alisema, chama tawala kitashirikiana na Serikali kutatua changamoto hiyo.

Alisema, baada ya kusikia malalamiko ya wananchi wa Muheza kuhusu kero ya Maji, chama kimesikia na kufika kujionea hali halisi pamoja na kutembelea vyanzo vya maji.

Amesema kwamba chama kwa kushirikiama na Serikali kitashughulikia kadhia hiyo kwa haraka huku akiwataka wananchi wa Muheza kuwa wavumilivu kwa Serikali yao.

Katibu huyo wa CCM Mkoa wa Tanga, ameeleza kuwa licha ya changamoto hiyo iliyojitokeza kupatiwa ufumbuzi wa haraka, wilaya ya Muheza itarajie kupata mradi mkubwa utakaowezesha kero ya maji kuwa historia.

"Tunamshukuru Rais azma yake ya kumtuma mama ndoo kichwani,Muheza wapo kwenye mradi wa miji 28 na watatumiwa Mil 40 kumaliza kabisa kadhia ya maji"alisema Suleiman Mzee Suleiman.

Wakati kukitolewa maelekezo hayo, Mkuu wa wilaya ya Muheza Juma Saidi ameahidi kufanyia kazi maelekezo hayo ya chama tawala CCM lengo likiwa kuhakikisha wananchi wanapata elimu.

Amesema kwamba, kwa wale ambao wako kwenye vyanzo vya maji hawatavumiliwa na wanapaswa kuondoka kwenye maeneo hayo.

"Hatutawavumilia, tunapata shida ya maji Muheza sababu vyanzo vingi watu wamegeuza sehemu za kufanya shughuli zao"alisema mkuu huyo wa wilaya ya Muheza Juma.

Awali Meneja wa maji Tanga Uwasa wilayani Muheza,Ramadhani Nyambuka amekiri uwepo wa changamoto ya maji kwa wananchi huku akiishukuru Serikali kwa kuhakikisha huduma ya maji inaimarishwa wilayani hapo.

Pamoja na hayo pia ameomba ushirikiano kwa wananchi katika kutunza vyanzo vya maji ili huduma kuweza kuwa endelevu.
Mwisho.


Pichani mkono wa  kulia ni Katibu wa CCM mkoa wa Tanga,Suleiman Mzee Suleiman akiwa na mkuu wa wilaya ya Muheza Juma Said wakitembelea vyanzo vya maji wilayani hapo.



 

No comments:

Post a Comment