Thursday, 11 May 2023

ZIARA YA DC KOROGWE JOKATE AHIMIZA UADILIFU BANDARI YA TANGA,,

 



Pichani ni Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Mkoani Tanga Jokate Mwegelo akihimiza suala la uadilifu na utendaji kazi kwa wafanyakazi wa Bandari ya Tanga huku akisema hatua hiyo italeta taswira nzuri na kulinda wateja wasipotee.

NA SOPHIA WAKATI,TANGA
MKUU wa Wilaya ya Korogwe Mkoani Tanga amehimiza suala la uadilifu kwenye utendaji kazi Bandarini akisema hatua hiyo italeta taswira nzuri na kulinda wateja wasipotee.

Mkuu huyo wa Wilaya alitoa rai hiyo juzi alipotembelea Bandari ya Tanga akisema Bandari na Viwanja vya ndege ndio malango makuu ya nchi hivyo lazima kuweka uadilifu ili kujenga uaminifu.

"Ili tuonekane wa maana lazima tuweke uadilifu kwenye utendaji kazi wetu,muonekano wa awali utakujengea uaminifu au kuonekana mpuuzi"alisema Jockate.

Katika ziara yake hiyo ya kikazi DC Jockate Mwegelo aliambatana na wafanyabiashara,AMCOS,baadhi ya taasisi za kifedha,watendaji,viongozi wa chama tawala na wale wa halmashauri za wilaya ya Korogwe.

Lengo la ziara hiyo ni kujionea utekelezwaji mradi mkubwa wa maboresho Bandari ya Tanga sanjari na wadau kutoka Korogwe kuona ni kwa jinsi gani wanaweza kunufaika.

Baada ya Mwegelo kupokea taarifa juu ya mradi huo uliyoigharimu Serikali ya awamu ya sita Shilingi 429.1 bilioni wadau walipata fursa ya kujadiliana mambo machache na uongozi wa Bandari ili tija kuweza kupatikana zaidi.

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Korogwe Vijijini Ally Waziri aliishauri Bandari suala la ajira kutoa kipaumbele kwa vijana wazawa badala ya kugawa kazi za kuajiri kwa Makampuni ambayo yatajipangia utaratibu wao.

"Mimi nilishawahi kuja hapa nikahoji mambo kadhaa, niliwahi kuelezwa kuna kampuni zinazoshughulika na ajira,hawa sijui kama wanaweza kuwachukua vijana wetu wanaweza kuja na watu wao na hili halitakuwa na afya"alisema Waziri.

Waziri alitumia fursa hiyo kumpongeza na kumshukuru Rais Dk Samia Suluhu Hassan kuwapatia Korogwe DC Jockate Mwegelo aliyemweleza kuwa kiongozi mwenye maono makubwa.

Miongoni mwa hoja nyingine za wadau zilizowasilishwa kwenye kikao hicho ni juu ya suala la ghama za usafirishaji mizigo kukosa uwiano ambapo Dar es Salaam na Mombasa zimedaiwa kuwa chini.

Wadau hao wapo waliosema wanapenda kutumia Bandari yao ila wanakwamishwa na jambo hilo ambalo katika ufafanuzi kutoka Bandari suala hilo lilionekana kuwahusu zaidi Shipping agent.

Hata hivyo imeelezwa kuwa hivi sasa huduma katika Bandari ya Tanga zimeimarika zaidi tofauti na awali ambapo kama wadau wataitumia kikamilifu kwa wingi wao wa mizigo ni dhahiri kuwa gharama zitapungua.

Imeelezwa kuwa kwa sasa Shipping agents wamekuwa wakileta Meli ndogo kutokana na mizigo iliyopo ambapo wanashindwa kuleta Meli kubwa wakihofiwa kupata hasara ya kutumia mafuta mengi.

Kutokana na hali hiyo wadau wakiwemo wakulima wa Mkonge wameshauriwa kuongeza nguvu katika kuitumia Bandari hiyo utaqatibu ambao unaaminika kuleta mabadiliko.

Majibu hayo yalimsukuma Mkuu wa wilaya Mwegelo kuahidi kuendelea kufanya hamasa kwa wadau wengi zaidi kuitumia Bandari ya Tanga huku akisema jukumu la kuwalinda wateja litabaki kwa Bandari wenyewe.

Mkuu huyo wa wilaya alitumia fursa hiyo kuwataka watendaji wa halmashauri kwenda kuandaa maeneo kuhakikisha yamepimwa na yawe na hati ili kunufaika na uwepo wa Bandari ya Tanga.

Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa wilaya maeneo hayo yanaweza kutumika kwa ajili ya uwekezaji wa aina mbalimbali ambapo wamiliki wataweka utaratibu wa kuyafanyia kazi.
Mwisho.

NA SOPHIA WAKATI,TANGA
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi CCM Korogwe Mjini, Thobias Nungu amesema kwamba, umefika wakati kwa Wataalam wa halmashauri kutenga maeneo kwa ajili ya uwekezaji Bandari kavu.

Nungu ametoa kauli hiyo juzi baada ya kupata wasaa wa kutembelea Mradi mkubwa wa kimkakati maboresho Bandari ya Tanga na kujionea fursa zilizopo.

Katika ziara ya kutembelea Bandari ya Tanga iliyoongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Korogwe,Jokate Mwegelo, Nungu alisema kama fursa ya uwepo Bandari itatumika vyema kuwekwa katikati ya sehemu ya wanaohitaji huduma za Bandari hiyo, Korogwe mji itanufaika.

"Kupitia Bandari ya Tanga kama tutatumia fursa ya kuiweka katikati ya sehemu ya wale wanaohitaji huduma Bandari ya Tanga yawezekana Mji wa Korogwe ukanufaika na kuongeza uchumi kwa wilaya,mkoa na taifa"alisema Mwenyekiti huyo wa Korogwe mji.

Aidha,Mwenyekiti huyo Nungu alisema, iko haja ya kuhimizwa uwekezaji wa nyumba za wageni wanaokuja kuchukua mizigo yao Bandarini kwa vile watalazimika kupata huduma za malazi,chakula na maji wilayani Korogwe.

Mwenyekiti huyo wa Chama tawala CCM,Pia amebainisha kuwa wilaya ya Korogwe ina miundombinu bora ya barabara zinazounganisha mikoa na nchi zenye kupitika vizuri kwa kipindi cha mwaka mzima.

Nungu amesema Korogwe ina kituo cha reli ambacho kinaweza kutumika kwa mizigo kusafirishwa kutoka Bandari ya Tanga kufikishwa mjini humo ili kuweza kuhifadhiwa.

Ameeleza kuwa, hatua hiyo itasaidia kuondosha msongamano Jijini Tanga ambapo kwa mizigo kuhifadhiwa Korogwe italeta tija kwenye eneo hilo kwa kuongeza kipato cha wananchi na hata kwa Serikali.

Pia ametumia nafasi hiyo kutoa ombi kwa mamlaka ya Bandari badala ya kuweka kila kitu Tanga likiwemo suala la kupakia na kuteremsha mizigo, sasa kutazama fursa nyingine Korogwe yenye eneo la kutosha kwa huduma hizo.

"Tuhamishe hizi huduma tuweze kuzisogeza Korogwe. Huduma za kijamii ziko za kutosha"alisema Nungu huku akitilia msisitizo kwa baadhi ya huduma za Bandari kuhamishiwa Korogwe ambayo kijiografia ni wilaya ambayo ipo katikati ya mkoa wa Tanga.

Alisema kwamba kukamilika kwa utekelezwaji Mradi wa Maboresho ujenzi Bandari ya Tanga kunatarajiwa kuleta mapinduzi makubwa ya kiuchumi kwa wananchi wa Mkoa huo na Taifa kwa ujumla wake.

Nae, Mkurugenzi mwendeshaji wa Shamba la Mkonge Gomba Wilayani Korogwe,David Mosha alisema kuwa asilimia 90 ya mizigo yao imekuwa ikisafirishwa kupitia Bandari ya Tanga.

Hata hivyo,Wengi wa wadau wa maendeleo walioshiriki ziara hiyo ya siku moja kutembelea Bandari ya Tanga iliyoandaliwa na DC Jokate Mwegelo walipongeza jitihada za kiongozi huyo kuwaunganisha sanjari na kupata fursa kuzungumza na uongozi wa Bandari kutoa maoni yao ili kuboresha shughuli zao za utendaji.
Mwisho.

NA SOPHIA WAKATI,KOROGWE
BENKI ya NMB tawi la Korogwe ina mpango mkakati wa kutoa mkopo wa mashine za kuchakata katani 'Korona'kwa wakulima wa zao la Mkonge ili kuwawezesha kulima kilimo chenye tija.

Hata hivyo imesema mchakato huo umeshaanza na kuwataka Wakulima wa zao la Mkonge kufanya subira katika kipindi hiki ambacho taratibu za kupatiwa Mikopo ya mashine za kuchakata Katani 'Korona' zikiwa zinafanyiwa kazi.

Kauli hiyo imetolewa juzi na Meneja wa benki ya NMB Korogwe, Lugano Mwampeta ambapo amewatoa hofu Wakulima hao wa Mkonge alipokuwa akizungumza na wadau wa zao la Mkonge,huku akiwasihi kuendelea kuwa wavumilivu wakati suala lao likiwa linashughulikiwa.

Katika mazungumzo yake hayo,Mwampeta alisema kuwa benk hiyo tayari imeshafanya utatiti kuwatembelea wakulima wa zao hilo la Mkonge lengo kuwawezesha kuwaondolea changamoto ya kuchakata katani.

Katika taarifa yake ufupi, Mwampeta alisema kwamba NMB ni benki pekee ambayo tangu awali imeonyesha nia ya dhati kuwakopesha Wakulima wilayani Korogwe mkoani Tanga.

Alisema, katika utendaji wake NMB imefanikiwa kutoa mikopo ya Matrekta na matrela yake kwa wakulima wa Mkonge huku lengo likiwa kuwawezesha kujikwamua kiuchumi.

Aidha,alibainisha kueleza kuwa mchakato wanaoendelea nao kwa sasa ni uchambuzi juu namna ambavyo wakulima watawezeshwa kupata mashine za Korona.

Alisema kwamba mchakato huo ingawa ni mrefu kidogo lakini unaendelea vizuri huku akiwasihi wakulima hao wa Mkonge kufanya subira wakati suala lao likiwa linashughulikiwa.

"Mimi niseme tu kwamba NMB tumekuwa wa kwanza kuwawezesha wakulima Korogwe,tumeshatoa matrekta na matrela na sasa tuko kwenye mchakato wa Korona"alisema Meneja huyo,Mwampeta huku akisisitiza uvumilivu kwa wakulima.
Mwisho.





No comments:

Post a Comment