Monday 5 June 2023

TPA TANGA YATUMIA MAONYESHO YA BIASHARA MWAHAKO KUELIMISHA WADAU KUTUMIA BANDARI,,,

Pichani ni Afisa Masoko wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari ya Tanga TPA.Habiba Godigodi akizungumza na waandishi wa habari kwenye maonyesho ya biashara kuhusu ushiriki wao lengo likiwa kutoa elimu kwa wadau mbalimbali.

NA SOPHIA WAKATI,TANGA
MRADI wa kimkakati ujenzi maboresho Bandari ya Tanga umeanza kuleta matokeo Chanya kwa jamii na nchi kwa ujumla wake huku ajira zikielezwa kuongezeka.

Afisa masoko wa Mamlaka ya usimamizi wa Bandari ya Tanga TPA.Habiba Godigodi ametoa taarifa hiyo jana alipoKkuwa akizungumza na waandishi wa habari kwenye maonyesho ya biashara Mwahako Jijini Tanga.

Habiba amesema Maboresho makubwa yaliyofanyika ni kupitia fedha kutoka Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dk Samia Suluhu Hassan hatua ambayo imeleta mafanikio makubwa kwa jamii na Tanzania kwa jumla wake.

Godigodi alisema ujio wa Meli kubwa umechangia ongezeko la ajira ambapo alibainisha kwamba tangu ujenzi huo kukamilika wamepokea Meli kubwa zaidi ya sita huku matarajio yakiwa kupokea meli nyingi zaidi jambo ambalo litaongeza ajira.

"Tumeshapokea meli kubwa sita tangu kukabidhiwa ghati na tunatarajia kupokea meli kubwa nyingi zaidi hivyo ni matumaini yetu ajira zitaongezeka kwa vile kazi zitakuwa nyingi" alisema afisa huyo wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari TPA.

Kwa mujibu wa Godigodi, Mamlaka ya usimamizi wa Bandari TPA imeshiriki Maonesho ya kumi (10) ya biashara na utalii Jijini Tanga ili kuweza kutoa elimu kwa wananchi na wadau mbalimbali juu ya huduma zinazotolewa na Bandari.

Alisema Bandari imekuwa ikihusika na huduma za kupokea na kusafirisha mizigo kutoka ndani na nje ya nchi huku akihamasisha wadau kuitumia Bandari ya Tanga.

"Bandari ya Tanga inatoa huduma bora, niwahakikishie wadau mbalimbali kwamba hakuna changamoto yoyote, karibuni kuitumia Bandari yenu" alisema Godigodi.

Mbali na hayo Godigodi amesema, kupitia Maonesho hayo TPA imekusudia kuifahamisha jamii juu ya uwekezeji uliofanywa na Serikali katika Bandari ya Tanga.

Alisema, Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan imewekeza zaidi ya Bil 429 kwa maboresho ya ujenzi Bandari ya Tanga.
Mwisho.

Pichani mkono wa kulia ni Afisa Masoko wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari ya Tanga TPA.Habiba Godigodi akiwa na Afisa Tehama,Ally Issaka wakiwa katika banda la maonyesho la TPA Mwahako jijini Tanga.

 

No comments:

Post a Comment