Saturday 5 August 2023

MKUTANO WA JUMUIYA YA MARIDHIANO NA AMANI TANZANIA JMAT MKOANI TANGA ULIKUWA HIVI,,,

Pichani ambaye amesimama ni Mwenyekiti wa JMAT Taifa, Alhaj Mussa Sallum Jijini Tanga kwenye Semina ya siku moja na Viongozi wa maridhiano na Amani iliyofanyika katika ukumbi wa YDCP akiwataka wanachama kuendelea kuimarisha amani iliyopo.


 NA SOPHIA WAKATI,TANGA

JUMUIYA ya maridhiano na Amani Tanzania (JMAT) imesema kwamba, haiko tayari kulumbana na chombo chochote huku ikitoa wito kwa viongozi wake wa mikoa kufanya kazi kwa kufuata miongozo na katiba yao.

Mwenyekiti wa JMAT Taifa, Alhaj Mussa Sallum akitoa wito Jijini Tanga kwenye Semina ya Viongozi wa maridhiano na Amani iliyofanyika ukumbi wa YDCP.

Katika Semina hiyo iliyowahusisha Viongozi wa Dini na watumishi wa Umma, Alhaj Mussa Sallum alisema, jumuiya ya maridhiano na Amani ni chombo kilichosajiliwa kisheria na kwamba katika utendaji wake hawahitaji kulumbana na chombo chochote kile.

“Mimi kama Kiongozi Mkuu wa jumuiya hii, nitoe wito kwa viongozi wetu mikoa yote hatuhitaji kulumbana na taasisi yoyote ila sisi tufanye kazi kwa mujibu wa katiba yetu,kwa mwongozo tulionao”alisema Alhaj Mussa.

Alhaj Mussa Sallum aliendelea kusema kuwa,iwapo kuna chombo au mtu ambaye anajihusisha na kuisaidia Serikali aendelee kufanya hivyo kwa taratibu zake huku akisisitiza kuwa JMAT itafanya kazi zake kwa  kuzingatia Sheria.

“Katibu chombo chako kimesajiliwa,huna haja ya kupambana na mtu au chombo chochote,fanya kazi kwa katiba uliyonayo na mwingine aliyesajiliwa kisheria atafanya kazi kama kama ambavyo Serikali inamtambua”alisema Mwenyekiti huyo wa JMAT Taifa.

Awali, Mwenyekiti wa Jumuiya ya maridhiano ya Amani Mkoani Tanga, Mbaraka Mwakivuma alisema kwamba,umoja wao umefanikiwa kufanya kazi na makundo yote huku Amani ikiendelea kuimarika.

Mwakivuma alisema kwamba, wanafanya kazi ya kudumisha Amani na viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini yakiwahusisha wakristo, waislamu pamoja na makundi ya jamii kama viongozi wa mila na tamaduni.

Alisema,harakati mbalimbali zimekuwa zikiendelea akitaja baadhi yake kuwa ni kukemea vitendo vya unyanyasaji kwa watoto, na kukemea mambo ambayo ni kinyume na maadili kama vile ushoga na usagaji.

Kwa upande wake Katibu wa JMAT Taifa,alielezea baadhi ya mafanikio yaliyopatikana tangu kuanzishwa umoja huo akisema,kupitia jukwaa hilo wameweza kutatua migogoro mbalimbali ambayo ingeweza kuhatarisha Amani.

Katibu huyo Daffa Juseicic Mhina alisema kwamba, wameielimisha Jamii kuhusu utii wa sharia za nchi hatua ambayo imesaidia kuzuia vitendo vya vurugu kujitokeza.

Mwisho.

Pichani ambaye amesimama ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya maridhiano ya Amani Mkoani Tanga, Mbaraka Mwakivuma akieleza kwamba,umoja wao umefanikiwa kufanya kazi na makundo yote huku Amani ikiendelea kuimarika.








No comments:

Post a Comment