Monday 1 January 2024

WANANCHI ZAID YA 600,000 WANATARAJIWA KUNUFAIKA NA MRADI MKUBWA WA MAJI MIJI 28,

Pichani ni Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira, Handeni Trunk Main (HTM),Mhandisi Yohana Mgaza akizungumza na waandishi wa habari  Ofisini kwake juu ya utekelezaji wa mradi mkubwa na wananchi wanaotarajiwa kunufaika..

NA SOPHIA WAKATI,KOROGWE

ZAIDI ya Watu 600,000 wanatarajiwa kunufaika na upatikanaji wa huduma ya Maji Safi na salama kupitia utekelezwaji Ujenzi Mradi mkubwa wa Maji wa Miji 28 ambao utazigusa Wilaya za Korogwe, Handeni, Muheza na Pangani zilizopo katika Mkoa wa Tanga.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira, Handeni Trunk Main (HTM), Yohana Mgaza alitoa taarifa wakaTi alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari Ofisini kwake.

Mgaza ambaye kitaaluma ni Mhandisi alisema, utekelezwaji mradi huo tayari umeshaanza ambapo chanzo cha Maji hayo itakuwa Mto Pangani kutoka kwenye Kijiji cha Mswaha Darajani wilayani Korogwe.

Mradi huo unatekelezwa na Kampuni ya M/s Jwil Infra Construction Limited na Kampuni Mshauri ni WAPCOS zote za nchini India ambapo wasimamizi Handeni Trunk Main kwa niaba ya Wizaya ya Maji.

Mhandisi Mgaza alisema kuwa fedha nyingi za Serikali zitatumika kwa ajili ya kufanikisha utekelezaji Mradi huo lengo likiwa kutimiza azma ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kumtua Mama ndoo kichwani.

Mgaza alisema kwamba, kwa wilaya hizo nne (4) za Pangani, Muheza, Korogwe na Handeni Mradi utagharimu Shiulingi Bilioni 200 ambapo Wataalam wa HTM watahakikisha unajengwa kwa viwango stahiki.

Akizungumzia zaidi shughuli za ujenzi wa mradi huo, Mgaza alisema kule kwenye chanzo ambapo ni eneo la Kijiji cha Mswaha Darajani kutajengwa Mtambo wa kuchuja Maji kabla ya kuanza kusambazwa.

Vilevile alisema kwamba,kazi kadhaa zimeendelea kufanyika akitaja ujenzi wa matenki ya kuhifadhia Maji huku mengine yakiwa kwenye hatua ya kuwekwa Zege ili kuyawezesha kuhifadhio Maji ya kutosha.

Pamoja na hayo Mgaza aliishukuru Serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassani kwa kuwezesha upatikanaji wa fedha ambazo leo zinawezesha utekelezwaji mradi huo mkubwa wa Maji.

Aidha Mgaza alisema ujenzi mradi wa Maji kwa Miji minne Mkoani Tanga utaongeza kipato cha Wananchi kwa vile Vijana watahitajika kwenye ujenzi huku akina Mama wakishiriki kupika na kuuza chakula.

Mwisho.


 

No comments:

Post a Comment