Pichani ni Mkuu wa wilaya ya Handeni,Wakili Albert Msando akiwaasa wahitimu katika hafla ya kufunga mafunzo kambi ya Mgambo kikosi cha 835 KJ kilichopo Kabuku wilayani Handeni mkoani Tanga.
NA SOPHIA WAKATI,HANDENI
WAHITIMU mafunzo ya Operesheni ya miaka 60 kujitolea kujenga taifa kikosi cha Mgambo JKT iliyopo wilayani Handeni wametakiwa kuyatumia vema mafunzo waliyopata huku wakiepuka kudanganywa kwa kushawishiwa ili kujiepusha kuingia kwenye vitendo vya uhalifu na hivyo kulisaliti Taifa lao.
Ushauri huo umetolewa na Mkuu wa wilaya ya Handeni,Wakili Albert Msando alipokuwa mgeni rasmi katika hafla ya kufunga mafunzo ya awali kwa wahitimu wa Mgambo JKT kikosi cha 835 KJ kilichopo Kabuku wilayani Handeni mkoani hapa.
Wakili Msando aliwaasa wahitimu hao akisema,wanapaswa kutumia vizuri mafunzo waliyopata na akiwasisitiza uadilifu na kukiishi kiapo walichoapa huku wakijilinda kwa kuepuka kushawishiwa na kutumikia kwenye uhalifu.
Alisema, vijana hao ambao ni jeshi la akiba wanategemewa kuwa walinzi wazuri wa Taifa lao na kwamba itapendeza wakiepuka kuingizwa kwenye ushiriki wa vitendo viovu na kwamba atakayediriki kufanya hivyo sheria haitasita kuchukua mkondo wake.
Aidha Msando amewaasa vijana hao juu ya matumizi bora ya mtandao akisema ukuaji wa teknolojia umesababisha watu wengi kuingia kwenye matumizi ya Simu selula ambapo wengine wamekuwa wakitumia vibaya na wengine vizuri.
Amesema,wahitimu wa Mgambo JKT wanapaswa kutumia vizuri teknolojia ili iweze kuwanufaisha katika maisha yao huku Taifa nalo likiweza kupata faida badala ya kuitumia visivyo.
"Tuwe makini katika matumizi ya mitandao tutumie kwa faida zetu na Taifa letu"alisema Wakili Msando huku akishauri wahitimu hao wa mafunzo ya awali JKT kwa kujitolea kuendelea kulelewa badala ya kuachwa wenyewe.
Aidha ametumia nafasi hiyo kwa kuzishauri halmashauri za wilaya kuangalia uwezekano wa kuwatumia vijana hawa katika eneo la ukusanyaji mapato akisema Handeni ilishaanza kufanya hivyo na imepata mafanikio makubwa baada ya kufanikiwa kukusanya kwa asilimia 109 huku mwaka wa fedha ukiwa haujaisha.
Naye Mwakilishi wa Mkuu wa Majeshi Kanali Ernest Elias amewapongeza vijana hao wahitimu kwa kuitikia wito na kujituma kupokea mafunzo hadi kuweza kufikia katika viwango bora.
Alibainisha kuwa Serikali inaendelea kufanya maboresho imetoa fedha kiasi cha Shilingi million 570 zilizowezesha kuimarishwa kwa miundombinu hali ambayo imesababisha vijana wengi kupata nafasi ya kujiunga na kikosi cha Mgambo JKT.
''Tunaishukuru serikal inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha nyingi million 570 kwenye kambi ya Mgambo JKT,kuwezesha kufanya maboresho ya mabweni kuwezesha kupokea vijana wengi zaidi ya 900''Alisema Mwakilishi huyo wa mkuu wa Majeshi.
Awali,Kamanda wa kikosi cha Mgambo JKT,Lutten Kanal Raimond Hafrey Mwanry alisema kwamba vijana hao walianza kujiunga na mafunzo yao Desemba 27 mwaka 2023 ambapo wameiva na wako tayari kulitumikia taifa lao.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment