Tuesday, 6 August 2024

MAONYESHO YA NANENANE 2024,YAIBUA WAKULIMA KUTOA CHANGAMOTO ZAO KWENYE SEKTA YA KILIMO,,



Pichani mkono wa kushoto ni mkulima wa zao la machungwa wilayani Muheza mkoani Tanga akiwa katika maonyesho mkoani Morogoro.

NA SOPHIA WAKATI,MOROGORO
WAKULIMA wa Matunda Wilayani Muheza Mkoani Tanga wameiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kuwapatia mashine ya kuchakata machungwa hatua ambayo itawaepusha na changamoto ya mazao yao kuoza shambani.

Wametoa Wito huo kwenye maonesho ya Kilimo nanenane yanayofanyika Mkoani Morogoro, ambapo Richard Ismail wa Kata ya Songa wilayani Muheza mkoani Tanga,ameomba kuangaliwa uwezekano wa kujengewa kiwanda kidogo ili kuondoa changamoto hiyo kwa wakulima.

Ismail alisema kwamba, katika wilaya yao wamekuwa wakizalisha kwa wingi machungwa ya aina mbili huku akitaja Msasa na Valencia ingawa hapo awali pia walizalisha aina ya Jafa. 

Alisema kuwa, katika Kilimo hicho licha ya wananchi wengi kuhamasika lakini bado wamekosa kunufaika kwa kiasi kikubwa kutokana na matunda wanayolima kuozea Shambani. 

"Tumefanikiwa kuzalisha kwa wingi Machungwa ila kwa ukdsefu wa mashine ama kiwanda kidogo,mengi huozea mashambani na hivyo tunapata hasara" alisema Mkulima huyo.

Pamoja na hayo ameishauri Serikali kupitia Halmashauri yao kuwatumia maafisa ugani katika kuwapatia elimu kabla mkulima hajapata hasara ya kwa wadudu kushambulia mazao yao na hivyo kuwaepusha na uwezekano wa kupata hasara.

Hata hivyo,Mkulima Ismail alielezea kuridhishwa kwake na hatua za haraka zinazoendelea kuchukuliwa na maafisa ugani katika kuwafikishia dawa wakulima wa zao la matunda.

Mbali na kuzungumzia biashara ya machungwa, Ismail alisema kuwa pia wamekuwa na utaratibu wa kuandaa miche na kuiuza kwa watu wanaohitaji  akisema katika kipindi cha mwaka 2022/23 waliandaa miche mingi huku akiwashukuru maafisa ugani kwa kuwapelekea madawa.

Kwa upande wa masoko kwa ajili ya kuuzia mazao yao,Ismail aliitaja mikoa ya  Dar es salaam, Mbeya, Pwani na nchi jirani ya Kenya ingawa alilalamikia changamoto ya madalali wanaoteremsha bei jambo ambali linaleta shida kwa mkulima na kukosa kipato stahiki.
Mwisho.

Pichani ni mkulima wilayani Muheza akiwa kwenye maonyesho ya nanenane 2024.

NA SOPHIA WAKATI,MOROGORO
WAKATI uzalishaji wa Zao la Mkonge katika Halmashauri ya Mji Korogwe ukiongezeka huku Wakulima wengi wakihamasika kushiriki Kilimo hicho, mavuno yamekuwa chini ya kiwango kutokana na kukabiliwa na changamoto ya mashine ya uchakataji wa zao hilo.

Kutokana na hali hiyo, Serikali imeshauriwa kuangalia uwezekano wa kuwawezesha Wakulima wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe kupata mashine hiyo 'Korona' hatua ambayo itawawezesha kushiriki Kilimo hicho kwa tija.

Mkuu wa idara ya Kilimo na Uvuvi wa Mji Korogwe, Ramadhani Amiri alisema kuwa kwenye mazao ya biashara wananchi wamehamasika katika kulima Mkonge ingawa wamekuwa wanakabiliwa na changamoto ya mashine ya uchakataji.

Alikuwa akishiriki maonesho ya Kilimo nane nane Mkoani Morogoro ambapo alieleza kuwa,iwapo Serikali itafanikiwa kuwawesesha wakulima kupata mashine hiyo ya Korona kwa ajili ya uchakataji uzalishaji utakuwa wenye kiwango stahiki na hivyo tija kuweza kuonekana.

Alisema kwamba, wengi wa wananchi wanaoshiriki Kilimo hicho wamekuwa wakitoka kwenye AMCOS akitaja ile ya Mgombezi na kwamba wakiwezeshwa uchumi wao utaimarika huku pato la Serikali nalo pia likiweza kuongezeka.

"Uzalishaji wa Mkonge umeongezeka, wakulima wanahamasika ila tuna changamoto ya mashine ya kuchakata Mkonge.Mavuno hufanyika chini ya kiwango" alisema Mkuu huyo wa idara ya Kilimo na uvuvi katika Halmashauri ya Mji Korogwe. 

Pamoja na hayo, Sekija alisema licha ya Korogwe kuwa Mji ila kuna maeneo ya kutosha kufanya uwekezaji akitaja suala la Viwanda vya matunda na kuwaomba wenye nia hiyo kuwekeza katika Halmashauri ya Mji huo wa Korogwe. 

"Wawekezaji wanakaribishwa...Korogwe ipo katikati na fursa ni nyingi kwa mfano watu wanaweza kufanya uwekezaji kwenye viwanda vya kuchakata matunda "alisema Sekija.

Sekija aliongeza kuwa hali ya miundombinu iliyoimarika akitaja barabara na mingineyo ni vitu ambavyo vinatoa fursa ya kumwezesha mwekezaji yeyote kuendesha shughuli anayohitaji pasipo kukabiliwa na changamoto ya aina yeyote.
Mwisho.



NA SOPHIA WAKATI,MOROGORO
HALMASHAURI ya Wilaya ya Handeni Mkoani Tanga imejidhatiti katika kutengeneza mazingira bora kwa Wafugaji wake hatua ambayo lengo lake ni kuwawezesha kupata mazao yenye ubora na hivyo tija kuweza kuongezeka.

Katika mikakati yao hiyo maeneo kadhaa yametengwa kwa ajili ya wafugaji zikiwemo hekta 22 zinazotumika kwa ajili ya kupata majani yanayotumika kama chakula cha mifugo hususani ng'ombe.

Mkuu wa idara ya kilimo  Ufugaji na Uvuvi Handeni Vijijini,Ibalila Chiza  anasema kuwa katika kuboresha sekta ya mifugo wanatekeleza zoezi la kuboresha Vinasaba kwa ng'ombe ambapo wanachagua ng'ombe bora wa kienyeji na kuwapandikiza na wale wa kisasa ili kupata matokeo bora.

Katika utaratibu huo, Chiza alisema wamefanikiwa kupata mbegu ya ndama wa miezi mitano akiwa na uzito 110 Kg hatua ambayo pia imesaidia kuongeza idadi ya wafugaji.

Hatua za namna hiyo zimeanza kuchukuliwa kwenye eneo la Msomera ambapi Halmashauri inaongeza nguvu ya ukusanyaji fedha kupitia mapato ya ndani kuboresha mifumo ya wafugaji

"Tumetenga maeneo na ranchi zipo kama tatu Handeni tunawakaribisha wawekezaji wa ndani waje kuwekeza kwenye mifugo"alisema Mkuu huyo wa idara ya Kilimo,Chiza. 

Ametaja faida zinazopatikqna kwa kutumia ng'ombe wa kisasa kuwa ni uzalishaji nyama na maziwa kwa wingi huku akitanabaisha kuwa upandikizaji ng'ombe kienyeji gharama zake ni zile za wastani.

Afisa huyo amemtolea mfano mmoja wa wakulima anayeitwa Shauri huko Kata ya Misima kwamba amepandikiza Ng'ombe 20 na 18 wamezaliwa na kwamba Mwaka mpya unaoanza zoezi litaendelea huku matarajio yakiwa kuwapoteza kabisa ng'ombe wasiokuwa na ubora.

Akizungumzia zao jingine la biashara wilayani Handeni kuwa ni Mkonge ingawa wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa.mashine ya.kuchakata zao hilo na kupata bidhaa ya nyuzi bora zinazohitajika sokoni.

Pia alisema, wamekuwa wakijishughulisha na kilimo cha zao la matunda ambayo huingizia fedha nyingi Halmashauri ambapo wangetamani kuwa na kiwanda cha kuongeza thamani matunda.

Pamoja na hayo kuna zao mama la mahindi asilia linqlotukika kwa chakula na biashara ambapo kuna mwekezaji mmoja mwenye kiwanda cha nafaka bado anahitaji mwekezaji eneo hilo.
Mwisho.

NA SOPHIA WAKATI,MOROGORO
MENEJA mradi wa Shirika linalojihusisha na shughuli za utunzaji wa mazingira TFCG, Simon Lugazo amesema kwamba, kwa hivi sasa wanaendelea kuisaidia jamii kujua namna ya kunufaika na Misitu yao kwa kufanya uvunaji endelevu ambao pia utawasukuma kwenye kutunza.

Lugazo aliyasema hayo juzi katika mahojiano maalum na Gazeti hili akisema, katika mradi wao huo wamepata ufadhili kutoka Jumuiya ya Ulaya huku wakishirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 

Mradi huo unatekelezwa katika wilaya za Handeni, Kilindi,  Mkinga na Pangani ambapo Lugazo alieleza kuwa maeneo hayo yanakabiliwa na changamoto ya uvunaji holela wa mkaa, migogoro ya mipaka, wakulima na wafugaji kukosa ushirikiano madhubuti.

Kuhusu ukosefu wa ushirikiano kati ya wakulima na wafugaji Lugazo alisema, upande mmoja wa wafugaji ulikuwa umesahaulika ambapo sasa wameanza kushirikisha il8 kuona kuwa mazingira ni sehemu ya maisha yao.

Elizabeth Fundi ni Mwananchi anayefanya kazi na mtabdao wa usimamizi misitu Mjumita alisema, wanashirikiana na TFCGgm ili kuleta suluhisho katika udumishaji wa misitu, kujengea uwezo kwa jamii zinazoishi jirani na misitu kwa kuwafundisha matumizi bora ya misitu,kuzalisha mkaa kwa njia nzuri usimamizi misitu.

Naye Zubeda Kihiyo alisema kwamba, kupitia Shirika la TFCG wamefanikiwa katika kuelimishwa namna ya kutatua migogoro na kuangalia kupinga ufugaji ndani ya misitu nk.

Alisema, elimu waliyoipata imeanza kuleta mabadiliko chanja kutokana na jamii kubadilika tofauti na ilivyokuwa hapo awali kwa vile wapo ambao wanazingatia suala zima la matumizi salama kwa misitu inayowazunguka.

Mwisho.





Pichani ni miongoni mwa wadau wa mazingira.



NA SOPHIA WAKATI,MOROGORO
HALMASHAURI ya Wilaya ya Lushoto Mkoani Tanga imejidhatiti katika kuwainua Wakulima wake baada ya kufanikiwa kupata mashine maalum ya kupima udongo ili kuzalisha mbegu bora zitakazowasaidia wananchi kuzalisha mazao yenye tija.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Ikupa Mwasyoge, alitoa taarifa hiyo jana katika maonyesho ya Nane nane yanayoendelea mkoani hapo ambapo alimshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha mchakato huo.

Mwasyoge alikuwa akihudhuria maonesho ya Kilimo nane nane huko Mkoani Morogoro yenye Kauli mbiu inayosema "Chagua Viongozi bora wa Serikali za mitaa kwa maendeleo ya kilimo,mifugo na uvuvi".

Alisema, kuwa Serikali inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Kilimo walitoa mafunzo kwa maafisa ugani ikiwa ni pamoja na kutoa mashine hiyo ya kupima udongo kwa Halmashauri yao.

Alisema udongo unapopimwa inasaidia katika zoezi la uzalishaji mbegu zenye ubora na hivyo wakulima kuzalisha mazao yenye ubora, akisisitiza kusema kuwa Serikali imejielekeza zaidi katika tafiti ili kuwawezesha wakulima kuendesha  kilimo kwa tija.

Pamoja na hayo Mwasyoge alisema, Serikali imewapatia fedha zilizowawezesha kujenga skimu za umwagiliaji huku maeneo mengine wakijenga mabwawa hatua ambayo inalenga kuwainua wakulima wake.

Aidha Kaimu Mkuu wa Idara ya Kilimo,mifugo na uvuvi wilayani Lushoto, George Medeye, alisema kwamba Jiografia ya Lushoto imewawezesha kulima mazao mbalimbali yakiwemo yale yasiopatikana kwenye maeneo mengine hapa nchini.

Alisema kwamba,wilaya yao imejikita zaidi katika matumizi ya teknolojia ili kuweza kunufaika huku akitanabaisha kwamba wamechukua zao la ngano kulifanya kuwa la mkakati ili kusaidia kuwainua wananchi kiuchumi na pia kuongeza mapato ya Serikali.

Kwa mujibu wa Mideyo vipaumbele vyao ni kuongeza tija kwenye uzalishaji Kilimo na Mifugo kwa kutumia mbinu za kisasa baada ya kupata huduma za ugani,akisema kuwa wanawawezesha wakukima kuzalisha muda wote baada ya kuboresha miundombinu. 

Ameishukuru Serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuwawezesha huku akisema kwamba wamekuwa wakifanya harakati mbalimbali kuhakikisha wakulima wanapata  masoko ya uhakika.
Mwisho.





No comments:

Post a Comment