Mratibu wa Mashindano ya Ulinzi Cup Sophia Wakati akikagua timu za soka Small Prison na Home Guard kabla ya kuanza mchezo wao katika uwanja wa soka Ziwani Pongwe Jijini Tanga |
Na Sophia Wakati, TANGA.
TIMU za soka Small Prison na Home Guard zimeaga Mashindano ya Ulinzi Cup baada ya kila mmoja kufungwa katika mchezo wa hatua ya mtoano inayoendelea kwenye viwanja vya Ziwani Pongwe Jijini Tanga.
Mashindano hayo yanaratibiwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga yakiwa na lengo la kutoa elimu kwa vijana kujiepusha na vitendo vya uhalifu katika jamii wanazoishi ikiwemo kuwa mabalozi wa amani kwenye maeneo yao
Katika mchezo wa awali wa ufunguzi wa mashindano hayo timu ya soka TFC waliigaragaza Home Guard bao 1-0 bao ambalo lilifungwa na Mohamed Saidi dakika ya 5 hya mchezo huo ambao ulikuwa na upinzani.Mratibu wa Mashindano ya Ulinzi Cup Sophia Wakati kushoto akitoa elimu kwa wachezaji wanaoshiriki mashindano hayo kuhusu lengo la mashindano hayo kuunga urafiki baina ya Polisi na Jamii
Huku mchezo wa pili uliochezwa Agosti 21 mwaka huu timu ya Chote FC waliweza kuwapigisha kwata maafande wa Jeshi la Magereza Small Prison bao 1-0 ambalo lilifungwa na Boniface Majere dakika ya 47.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mashindano hayo,Diwani wa Kata ya Pongwe (CCM) Mbaraka Sadi alilipongeza Jeshi la Polisi kwa kazi kubwa anayoifanya kwa kuhakikisha Jeshi la Polisi linakuwa karibu na Jamii jambo ambalo ni muhimu katika kuhakikisha kuimarisha ulinzi.
Mbaraka alisema kwamba kufanyika kwa mashindano hayo katika maeneo mbalimbali yanasaidia na kuwawezesha vijana kuweza kuyatumia kama njia muhimu ya ajira,kujenga afya pamoja na kusaidia kuwaondoa vijana kwenye masuala ya uhalifu na dawa za kulevya na wanaamini mashindan hayo yatakuwa chachu kubwa ya kuinua vipaji vya wachezaji.
Naye kwa upande wake Mratibu wa Mashindano hayo Sophia Wakati alivitaka vilabu vinavyoshiriki kwenye mashindano hayo kuhakikisha wanazingatia sheria 17 za mpira wa miguuu zilizowekwa ikiwemo kuacha kuwachukia waamuzi.
“Lengo la Mashindano hayo ni kujenga undugu baina ya Jeshi la Polisi na Jamii lengo kujenga urafiki msijengeane chuki hakikisheni mnacheza kwa kuzingatia nidhamu ambayo itakuwa chachu ya mafanikio kwenye jambo lolote lile lakini msiwachukie waamuzi kutokana na kwamba wakati mwengine kunakuwa na makosa ya kibinadamu”Alisema
Mwisho.
No comments:
Post a Comment