Thursday 29 August 2024

USAJILI WA TANGA CITY MARATHON 2024 KUFANYIKA KWA MTANDAO "ONLINE"

Waandaaji wa Mashindano ya Riadha ya Tanga City Marathon wakionyesha tisheti zitakazotumika kwa washiriki watakaoshiriki mashindano hayo msimu huu mara baada ya kuzungumza na waandishi wa habari Jijini Tanga kwenye ukumbi wa Tanga Beach Resort


# Usajili 'Tanga Marathon' 2024 kufanyika kwa mtandao 'Online'.

# Hamasa yatolewa kwa Wadau kuongeza nguvu udhamini mbio hizo, ni ili kuweza kunufaika na fursa zilizopo katika kuweza kujikwamua kiuchumi.

TANGA: MASHAKA KIBAYA 
MASHINDANO ya Riadha 'Tanga City Marathon 2024' yamekuja kivingine msimu huu, ambapo Usajili kwa washiriki wake utafanyika kwa njia ya mtandao 'Online' kupitia marathon. imartgroup.co.tz

Msemaji Kamati ya Mashindano hayo, Fatma Mbinga, akizungumza na waandishi wa habari jijini Tanga katika Tanga Beach Resort alisema kila kitu kimekamilika kwa upande wa zawadi kwa washindi,

Hata hivyo amebainisha kwamba mashindano hayo yamekuwa endelevu kufanyika kwa mwaka huu ni msimu wa nane (8) na wadau mbalimbali kujitokeza kushiriki. 

Fatma alisema, kwa mwaka huu usajili wa kumwezesha mtu kushiriki Tanga Marathon utafanyika kupitia njia ya mtandao huku akibainisha kuwa wamekuja kivingine na zawadi ni zenye kuvutia kwa washindi mbio hizo.

"Tunataraji Mbio zitakuwa tarehe 22/09/2024 leo tunatangaza jezi yetu ambayo ni nzuri, Tshirt yetu hii ina nafasi kubwa ya kufanya udhamini"alisema Bi Mbinga huku akitanabaisha kwamba medali zitatolewa kuanzia washindi wa mbio za Kilomita 5,10 na 21.

Aidha amesema kwamba, kwa mwaka huu 'Tanga Marathon' imejipanga kurejesha fadhila kwa jamii kwa kusaidia uimarishaji miundombinu ya elimu hususani madawati.

Naye Katibu wa mchezo wa riadha Mkoani Tanga, Hassan Tuano alisema kwamba, mbio za Tanga Marathon kwa mwaka huu zitakuwa zile za kihistoria ,akiwasihi washiriki wa ndani na nje kuja kushiriki ili kujifunza mambo mbalimbali yenye tija.

Tuano alisema kwamba, kufanyika kwa mbio hizo itakuwa fursa adhimu kwa wanaTanga hususani Wajasiriamali akiwataja mama lishe kuuza chakula na biashara nyjngine ili kuweza kujiingizia kipato.

Pia Mwenyekiti wa chama hicho cha riadha Mkoa wa Tanga, Bi Sophia Wakati, alitoa wito kwa wadau kujitokeza kwa wingi kufadhili mchezo huo na mingine ya aina hiyo inayokuwa ikifanyika katika mkoa huo wa Tanga. 

Bi Wakati alisema kwamba,kwa kufanya udhamini Chama cha riadha itatoa fursa kwao kujifunza mambo mbalimbali huku wakinufaika na fursa za uwekezaji zilizoandaliwa na Serikali yao katika mkoa huo uliopo pembezoni mwa Bahari ya Hindi. 

Tayari Kampuni ya Bima ya Bumaco, iMart Group Ltd na Tanga Beach Resort zimejitokeza kudhamini mashindano ya Tanga Marathon Mwaka 2024.
Mwisho.


No comments:

Post a Comment