NA SOPHIA WAKATI,HANDENI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, amesema Wizara ya Maji kutoka kuwa Wizara ya lawama sasa imekuwa ya mfano kwa utekelezaji miundombinu ya maji nchini.
Hata hivyo,amesema kutokana na kufanya kazi kubwa na nzuri ya kuhakikisha upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama yanapatikana kwa watanzania wote.
Ameyasema hayo huku akiipongeza katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la Mradi wa Maji wa Miji 28 kwa miji ya Handeni, Korogwe, Muheza, na Pangani, iliyofanyika katika eneo lilipojengwa tenki la maji Mkombozi, Mtaa wa Vibaoni, katika wilaya ya Handeni.
Dk. Samia Suluhu Hassan alisema kuwa, mwaka 2021 aliwasukuma sana huku akiwataka kufanyankazi kwa bidiii na kubainisha kwamba kuanzia kipindi cha mwaka 2022 Wizara ya Maji inafanya vizuri sana.
Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ameeleza kuwa, Serikali itaendelea kuhakikisha kwamba kunakuwepo upatikanaji wa fedha kwa miradi ya maji, huku akiwataka watendaji wa Sekta ya Maji kuendelea kufanya kazi kwa bidii.
"Kazi yangu mimi ni kutafuta fedha, na kazi yenu ni utekelezaji. Nawapongeza watendaji wote wa Sekta ya Maji, endeleeni kuchapa kazi." amesema Rais Samia ziara yake wilayani Handeni mkoani Tanga.
Awali, akizungumza mbele ya Rais, Waziri wa Maji,Jumaa Aweso alisema kwamba Wizara ya Maji imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kutokana na ushirikiano wanaoupata kutoka kwa Rais Samia, akisema miradi mingi imeweza kutekelezwa kwa wakati kutokana na utayari wa Rais Samia kuruhusu fedha ya utekelezaji wa miradi hiyo.
Mradi wa maji wa Miji 28 kwa mkoa wa Tanga unatekelezwa na Mkandarasi JWIL Infra Ltd na unasimamiwa na Kampuni ya WAPCOS, zote kutoka India. Mradi huo unatarajiwa kugharimu Dola za Kimarekani milioni 81.
Amesema mradi huo unahusisha ujenzi wa kidakio cha maji (intake) katika Kijiji cha Mswaha, Wilaya ya Korogwe, ujenzi wa chujio la maji (treatment plant) katika Kijiji cha Tabora, Korogwe, ujenzi wa matenki nane ya maji pamoja na ulazaji wa bomba lenye urefu wa kilomita 188.
Hadi sasa utekelezaji wa mradi huu umefikia asilimia 60, ambapo mabomba yenye urefu wa kilomita 140 yameshalazwa, tenki la maji lenye ujazo wa lita milioni 2 katika Mtaa wa Vibaoni, Wilaya ya Handeni, limekamilika, na tenki la kuhifadhi maji lenye ujazo wa lita 300,000 katika Kijiji cha Ubangaa, Wilaya ya Pangani, limekamilika.
Alibainisha kueleza kuwa Matenki mengine ya maji katika vijiji vya Bongi, Segera, Kwafungo, Kilulu, Madanga, na Boza yako katika hatua tofauti za utekelezaji mradi huo wa kitaifa.
Mradi huu unatarajiwa kukamilika ifikapo Desemba 2025 na utawezesha upatikanaji wa maji kwa zaidi ya wakazi 860,000 wa vijiji 161 vya Wilaya za Korogwe, Handeni, Muheza, na Pangani.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment