NA SOPHIA WAKATI,MKINGA
SERIKAL kupitia Wizara ya Maji imekusudia kutekeleza mradi mkubwa wa Maji Mkinga – Horohoro, utakaotumia chanzo cha Bwawa la Mabayani kwa lengo la kumaliza tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi katika maeneo ya mwambao wa Bahari ya Hindi mkoani Tanga.
Hayo yamethibitika kupitia mpango mkakati uliowekwa bayana kupitia ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan ambaye aliweka jiwe la msingi kwenye mradi huo wa Maji wa Mkinga – Horohoro uliopo katika Wilayani Mkinga, kwenye mkoa wa Tanga.
Mradi huo unatarajiwa kugharamiwa na fedha za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania fedha kutoka Mfuko wa Taifa wa Maji ambapo kiasi cha Shilingi bilioni 35.47 zitatumika.
Katuka taarifa yake kwenye hafla hiyo, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso alisema, wataalam wanaotekeleza mradi huo hawatasubiri mabomba yote yafike eneo la mradi 'site', isipokuwa wataendelea na kazi kwa kadiri mabomba yatakavyofika ili kukamilisha mradi kwa wakati.
Awali Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Mwajuma Waziri alisema kuwa, mradi huo ulio chini ya Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) mkandarasi ni Kampuni ya STC Construction Ltd, ulianza novemba 5, 2022 unatarajiwa kukamilika 5 Oktoba, 2025.
Mhandisi Mwajuma alisema kuwa Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni 35.47 kwa ajili ya mradi huo, huku tayari zaidi ya shilingi bilioni 11.32 zikiwa zimeshalipwa kwa mkandarasi anayehusika
Alisema, kwa muda mrefu, wakazi wa vijiji 37 vilivyopo wilayani Mkinga wamekuwa wakikabiliwa na changamoto kubwa ya maji wakitumia yake yenye chumvi, hali ambayo imechangia kuathiri shughuli za kila siku za uzalishaji.
Maji hayo wamekuwa wakitumia kwa matumizi ya nyumbani na kilimo na pindi mradi utakapokamilika unatarajiwa kuboresha huduma ya maji safi na salama kwa wananchi zaidi ya 57,334 wa kata 10 katika vijiji 37 vilivyopo pembezoni mwa barabara ya Tanga - Horohoro pamoja na wananchi wa eneo la Horohoro lililopo Mpakani mwa Tanzania na Kenya.
Kukamilika kwa ujenzi wa mradi huo utakuwa ukombozi mkubwa kwa wananchi wa Mkinga ambao watakiwa wakipata maji safi na salama na hivyo kurahisisha utekelezaji wa majukumu mengine ya uzalishaji mali.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment