Wednesday, 21 October 2026

COPRA YAJIPANGA KUONDOA CHANGAMOTO YA SOKO LA MAZAO KWA WAKULIMA

 

PICHA NI: Kaimu Mkuu wa Kanda ya Kaskazini wa COPRA, Fahamia Selemani akizungumza katika mdahalo wa wadau wa kilimo maonyesho ya chakula jijini Tanga.

NA SOPHIA WAKATI,TANGA

SERIKALI kupitia Wizara ya Kilimo, kwa kushirikiana na Wakala wa Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA), imeanza kuweka mikakati ya kuongeza thamani ya mazao ya nafaka mchanganyiko na kutafuta masoko ya uhakika ili kuwawezesha wakulima kunufaika zaidi na kilimo.

Hatua hiyo inalenga kukabiliana na changamoto za masoko zinazowakabili wakulima, ikiwemo kupoteza mazao kutokana na kukosa manunuzi, hali inayosababisha baadhi ya mazao yao kuoza yakiwa shambani.

Kaimu Mkuu wa Kanda ya Kaskazini wa COPRA, Fahamia Selemani, ametoa Kauli hiyo wakati wa mdahalo ulioshirikisha wadau mbalimbali katika maonyesho ya Chakula uliojadili masuala ya kilimo na masoko ya mazao.

Wakichangia mada katika mdahalo huo, Saumu Kipande, mkulima kutoka Malindi wilayani Lushoto, alilalamikia ukosefu wa masoko, akisema changamoto hiyo imechangia kuwasababishia mazao yao kuoza shambani kutokana na kukosa wanunuzi.

Nae Anisia Mauya mkulima kutoka Lushoto amelalamikia kukosa soko la uhakika inasababisha bidhaa ikiwemo mbogamboga kuozea shambani.

Aidha,watafiti kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) wameeleza mikakati ya kuleta teknolojia mbalimbali za uzalishaji na kuongeza thamani ya mazao ili kuimarisha usalama wa chakula na kuongeza manufaa ya kiuchumi kwa wakulima hapa nchini.

Mtafiti wa TARI, Joseph Mzunda, anayefanya kazi kituo cha Naliendele, alisema taasisi hiyo inaendelea na utafiti wa mazao mbalimbali, ikiwemo zao la tende, kwa kuanza na mikoa ya Dodoma na Singida yenye hali ya hewa ya joto na mvua chache.

Alisema tayari zimeingizwa mbegu aina nne za tende ambazo zimeanza kufanyiwa majaribio ili kubaini aina inazoweza kufanya vizuri mazingira ya mikoa hiyo.

Alibainisha baada ya kubaini aina zinazofaa, utafiti unaweza kupanuliwa kwa maeneo mengine, huku akieleza kuwa utafiti wa kawaida unaweza kuchukua hadi miaka 10, lakini matumizi ya teknolojia za kisasa yanapunguza muda huo hadi miaka sita au saba.

Aliongeza kuwa umwagiliaji unaweza kusaidia kufupisha mzunguko wa uzalishaji, huku akieleza kuwa kwa sasa watafiti wapo katika mchakato wa kukusanya takwimu na watazungumza zaidi baada ya takwimu hizo kukamilika.

Alisema wananchi wanapaswa kuwa na matumaini wakati watafiti wakiendelea na kazi ya kubaini aina za tende zitakazofanya vizuri katika maeneo yaliyolengwa.

Kuhusu umuhimu wa zao hilo, Mzunda alisema tende zina faida za kiuchumi na kiafya, zikiwemo virutubisho vinavyosaidia mwili, ubongo na mifupa, huku akieleza kuwa zao hilo linaweza kuwa chanzo cha chakula na kipato.

Kwa upande wake, mtafiti wa TARI, Gasper Ndumiliko, alisema taasisi hiyo imejipanga kuwaletea wananchi na washiriki wa maadhimisho hayo teknolojia mbalimbali zinazohusiana na uzalishaji wa chakula.

Alisema teknolojia hizo zinajumuisha matumizi ya mbegu bora na mbinu za kisasa za uzalishaji, ambazo ni muhimu katika kuongeza tija na kuhakikisha wakulima wanazalisha chakula cha kutosha.

Ndumiliko asema, teknolojia za mbegu bora zinazotolewa kupitia vituo vya utafiti vilivyopo nchini zinalenga kuimarisha uzalishaji wenye tija na kusaidia wakulima kupata chakula cha kutosha.

Alisema, watafiti wamewasilisha teknolojia za kuongeza thamani ya bidhaa mbalimbali za kilimo, hatua inayolenga kuongeza thamani ya mazao kiuchumi na kupunguza hasara zinazotokana na upotevu wa mazao.

Alisisitiza kuwa matumizi ya teknolojia hizo ni muhimu katika kuimarisha uzalishaji wa chakula na kuongeza manufaa ya kilimo kwa wakulima.
Mwisho.








No comments:

Post a Comment