Friday, 6 November 2026

SIKUKUU YA MAVUNO YAKUMBUSHA WAKRISTO KUMSHUKURU MUNGU KWA MAFANIKIO

 

NA SOPHIA WAKATI, TANGA

MCHUNGAJI wa Kanisa la KKKT Usharika wa Makorora, Martin Mweta amesema Sikukuu ya Mavuno inawakumbusha Wakristo kutoa sehemu ya mafanikio yao kwa Mungu kama ishara ya kumshukuru kwa baraka walizozipata. 


Amesema Sikukuu hiyo ya Mavuno ni wakati ambao Mungu anawakumbusha waumini kutoa sehemu ya kile kilichoongezeka katika maisha yao, ikiwemo mafanikio yanayotokana na kilimo, ufugaji na biashara.


Amesema hakuna kosa kubwa ambalo wanadamu wanaweza kufanya kama kumsahau Mungu katika kipindi cha mafanikio, akiwataka Wakristo kuendelea kudumisha uhusiano wao na Mungu kwa kutoa mavuno mazabuni.


Mchungaji Mweta amesema kuleta mavuno mazabuni ni kuonyesha kuwa kuna mahusiano mazuri kati ya mwanadamu na Mungu, huku kukiwa ni njia ya kumshukuru na kumuomba awajalie mafanikio mengine.


Amesema Wakristo wanapaswa kukaa kama familia na kuangalia kile kilichozidi katika mafanikio yao ili kutoa sehemu ya ziada hiyo kwa Mungu, jambo litakalowasaidia kupata mafanikio zaidi.


Naye mgeni rasmi katika Sikukuu ya Mavuno ya Kanisa la KKKT Usharika wa Makorora, Wakili Nashon Mwakihaba, amesema Wakristo kutotoa mavuno makanisani ni kuvunja mahusiano yao na Mungu.


Amesema kutoa mavuno ni sehemu muhimu ya kudumisha uhusiano huo, akiwataka waumini kuendelea kutimiza wajibu wao wa kumshukuru Mungu kwa mafanikio wanayoyapata katika maisha yao.


Mchungaji Mweta amesema kuanzia Jumanne kanisa limeaanza kupokea mavuno kutoka kwa waumini wanaotaka kutoa sehemu ya mafanikio yao kuelekea Sikukuu ya Mavuno itakayofanyika Jumapili, tarehe 8.


Amesema maandalizi hayo yanatoa nafasi kwa waumini kujiandaa na kutenga sehemu ya mafanikio yao kwa ajili ya kupeleka mazabuni wakati wa sikukuu hiyo.

Mwisho.










No comments:

Post a Comment