Monday, 27 March 2017

RC TANGA,AKIFUNGUA NYUMBA 10 ZILIZOJENGWA NA TAASISI YA BENJAMINI MKAPA KWA AJILI YA WATUMISHI WA SEKTA YA AFYA LUSHOTO,,

NA SOPHIA WAKATI,LUSHOTO
TAASISI isiyokuwa ya kiserikali ya Benjamini Mkapa maarufu yenye maskani yake jijini Dar es alaam imetumia kiasi cha sh 484 milioni kwa ajili ya kufanikisha ujenzi wa nyumba kumi (10) za watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Lushoto ambao wamekuwa wakiwajibika kwenye sekta ya afya lengo likiwa kusaidia uboreshaji wa huduma.

Taarifa hiyo ilitolewa na mhandisi Immanuel  Festo Yohana ambaye alisema kuwa ujenzi wa nyumba hizo ulianza hapo Aprili 22,2015 na kukamilika April 22,2016 ambapo nyumba hizo zimejengwa katika vituo vya afya na zahanati mbalimbali wilayani hapo lengo likiwa kuondoa changamoto iliyopo.

Alisema hatua hiyo itawezesha watumishi kuishi maeneo salama na hivyo kufanikisha mchakato wa utoaji huduma bora kwa wananchi huku akiwataja wanufaika kuwa ni kituo cha afya cha Mnazi na Zahanati za Mdala,Bwelowi,Makose na Zahanati ya Makanya ambapo miundombinu hiyo imekamilika.

Dk. Adelina Saguti kutoka taasisi ya Benjamini Mkapa Foundation alisema kuwa katika ujenzi huo wameshirikiana na benki ya Dunia kupitia mpango wa kupiga vita magonjwa yasiyoambukiza huku wakishirikiana na serikali kuboresha huduma za afya ambapo wamekuwa wakitekeleza jukumu hilo tangu mwaka 2011.

“Sisi tunafadhiliwa na benki ya Dunia inayopambana na magonjwa yasiyoambukiza,nyumba kumi zimejengwa wilayani Lushotoi katika vituo vitano ambapo umeme wa mfumo wa jua umekuwa ukitumika kwenye nyumba nane huku nyingine zikitumia umeme wa kawaida”alisema Dk. Saguti.

Dk. Saguti amesema kuwa mpango wao huo umelenga kuondosha changamoto mbalimbali kwenye sekta ya afya hususani kwenye maeneo ya vijijini hatua ambayo itasaidia tija kupatikana huku akitanabaisha kuwa katika mkoa wa Tanga mradi umetekelezwa wilaya za Handeni,Korogwe mji,Lushoto na Kilindi.

Vilevile Dk Saguti alisema kuwa mbali na msaada huo pia wamefanikiwa kutoa mafunzo mbalimbali kwa watumishi wa sekta ya afya hatua ambayo itawawezesha kumudu kujiendeleza na hivyo kutekeleza majukumu yao ya kuwahudumia wananchi kwa ufanisi na tija na hivyo kuboresha na kuimarisha nguvu kazi iliyopo.

Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Lushoto,Lukas Shemndolwa ameishukuru taasisi ya Benjamin Mkapa kwa jitihada zake za kusaidia sekta ya afya huku akitanabaisha kuwa kwenye eneo hilo wanakabiliwa na upungufu wa nyumba 200 kwa ajili ya watumishi ambapo sasa kero inapungua.

Shemndolwa alisema kwamba kupatikana kwa nyumba hizo ni sehemu ya ukombozi kwa halmashauri ya wilaya ya Lushoto na kwamba kutawawezesha watumishi kuishi jirani na maeneo yao ya kazi na hivyo kuwahudumia wananchi kwa ufanisi  hatuya ambayo itasaidia kuleta mafanikio kwa jamii.

Nae Mganga kiongozi kituo cha afya Mnazi,Azizi Nanjasye akishukuru amesema kwamba wanakabiliwa na changamoto ya jengo la upasuaji ambapo wamekuwa wakilazimika kusafiri umbali wa zaidi ya kilomita 20 kufika makao makuu ya wilaya kwa ajili ya kuwapeleka wagonjwa kwa huduma ya upasuaji.

Akizungumza na mkurugenzi wa Blog hii mwanaisha Ally mkazi wa Mnazi alilshukuru taasisi hiyo na kueleza kwamba nyumba hizo zimetolewa muda muafaka kwa sekta hiyo ya afya ambapo watumishi wataondokana na kutembea umbali mrefu kutoa huduma ya matibabu.



Mwisho.
 







 Pichani mwanamke mkono wa kulia ni Dk. Adelina Saguti kutoka taasisi ya Benjamini Mkapa Foundation akimkabidhi mkuu wa mkoa wa Tanga,Martine Shigela cheti cha nyumba 10 zilizojengwa na taasisi hiyo ili kuwaondolea changamoto ya upungufu  nyumba watumishi.
 RC Tanga mara baada ya kufungua akisoma ujumbe ulioandika,,


 Pichani ni Mganga kiongozi wa kituo cha afya Mnazi,Azizi Nanjasye akishukuru huku akieleza kwamba wanakabiliwa na changamoto ya jengo la upasuaji ambapo wamekuwa wakilazimika kusafiri umbali wa zaidi ya kilomita 20 kufika makao makuu ya wilaya kwa ajili ya kuwapeleka wagonjwa kwa huduma ya upasuaji.

Nyumba zilizojengwa na taasisi ya Benjamin Mkapa mara baada ya kufunguliwa na kukabidhiwa

No comments:

Post a Comment