Pichani kati kati ambaye amevaa sare ya polisi ni kamanda wa polisi mkoa wa Tanga,Benedict Wakulyamba na kushoto ni Ofisa upelelezi wa mkoa huo,Amedeu Tesha na kulia ni mlinzi maalum askari kitengo cha FFU,Gasper jana ofisini kwake akiwaonyesha waandishi wa habari ambao (hawapo pichani) silaha zote nne 4 za kutengeneza ambazo zinasadikiwa kutumika katika matukio mbalimbali ya kijambazi likiwemo la tukio la kuvamia nyumba wakiwa na silaha,mapanga na kumuua Mohamed Ally huko wilayani Kilindi.
NA SOPHIA WAKATI,TANGA
JESHI la Polisi mkoani Tanga linawashikilia watu wanne akiwemo
Yohana Sendeu (41)mkazi wa Kibaigwa mkoani Dodoma na Elisha Isaya (24) mkazi wa Gairo Morogoro wanaosadikiwa kuwa majambazi baada ya
kupatikana na Silaha mbili moja aina ya Shortgun na nyingine Pistor ambazo
zimetengenezwa kienyeji zinasadikiwa kuwa zilitumika kwa matukio ya
uhalifu.
Hata hivyo imeelezwa kukamatwa kwa watuhumiwa hao ni baada ya tukio la lililotokea kitongoji
cha Msaneni huko kijiji cha Kwekivu wilayani Kilindi ambapo Mohamedi Ally alivamiwa
nyumbani kwake na majambazi hayo na kufanikiwa kumpiga risasi kwa kutumia silaha
aina ya Gobore kwenye ubavu wa upande wa kushoto hadi kumuua.
Kamanda wa Polisi mkoani Tanga,Benedict Wakulyamba
amethibitisha kutokea kwa tukio hilo akisema watuhumiwa hao walikamatwa huko
katika kijiji cha Msaneni,Kwekivu wilayani Kilindi ambapo Yohana Sendeu ni
mkazi wa Dodoma na Elisha Isaya mkazi wa Gairo Morogoro wote wanaendelea
kushikiliwa.
Kamanda Wakulyamba alisema katika mahojiano na polisi
watuhumiwa hao walionyesha silaha mbili moja ikiwa gobore na nyingine Pistor
ambazo zote zilitengenezwa kienyeji zikitumia risasi za Shotgun ambapo zilikuwa
zimefichwa porini baada ya kutumika kwenye tukio la mauaji lililokuwa limefanyika.
Alisema kwamba katika mahojiano hayo na
watuhumiwa hao pia yaliwezesha kupatikana watu wengine wawili ambao ni Omari Selemani
maarufu ‘Chang'oma Dipochi’ (39) mkazi wa Chamtui Handeni na Salum Selemani maarufu Chang'endo (54) ambaye
ni mkazi wa Chamtui kwenye wilaya hiyo ya Handeni mkoani Tanga.
Aidha,ameitaja Silaha aina ya Shotgun ambayo
imekamatwa kuwa ni ile yenye nambari MG 873 A ambapo watuhumiwa wanaodaiwa
kuhusika kwenye matukio ya mauaji huko Tanga na Dodoma wote wanne wakiwa
wanaendelea kushikiliwa na polisi uchunguzi huku ukiwa unaendelea.
“Watuhumiwa wote wanaendelea kushikiliwa polisi kwa
mahojiano na uchunguzi utakapokamilika watafikishwa mahakamani ili kuweza
kujibu mashataka yatakayokuwa yakiwakabili”alisema kamanda huyo wa Polisi
mkoani Tanga huku akiwasihi raia wema kuendelea kushirikiana na jeshi la
polisi.
Katika tukio jingine kamanda Wakulyamba alisema kuwa huko
kwenye mtaa wa Mtakuja kijiji cha Mkalamo tarafa ya Mkwaja wilayani Pangani
amekamatwa Yusuph Ally (19) mkazi wa Handeni akiwa na silaha aina ya Pistor
iliyotengenezwa kienyeji ikiwa na risasi nne na mtuhumiwa anachunguzwa.
Alisema kuwa katika tukio hilo mara baada ya uchunguzi wa
polisi kukamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani kwa taratibu za sheria
kuchukua mkondo wake ambapo pia kamanda huyo wa polisi mkoani Tanga alitumia
fursa hiyo kuzungumza na wanahabari kutahadharisha usalama wa barabarani.
Wakulyamba alisema ingawa barabara ya kutoka Mombo kwenda
Lushoto iliyokuywa imezuiliwa kutumika kwa sasa imefunguliwa lakini iko haja
kwa wasafirishaji kuchukua tahadhari ya usalama kutokana na ukweli kwamba bado tathimini
na hatua za kufanya ukarabati unaendelea kufanyika.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment