NA SOPHIA WAKATI,MUHEZA
KAMANDA wa Polisi mkoani Tanga,Benedict Wakulyamba ameitaka
jamii kuutumia vyema Usafiri wa bodaboda na bajaji badala ya kuvunja sheria kwa
kuutumia kusafirisha bidhaa haramu na za magendo jambo ambalo litasababisha
kuchukuliwa hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kufungwa jela.
Kamanda huyo wa Polisi alitoa rai hiyo juzi alipokuwa
akifungua mafunzo kwa waendesha bodaboda wilayani Muheza kwenye hafla
iliyofanyika ukumbi wa Tarecu akisema kuwa biashara hiyo iliyorasimishwa
inapaswa kuonwa kama zilivyo kazi nyingine kwa wahusika kuziheshimu ili
kujijengea heshima kwa jamii.
Katika mafunzo hayo ya siku saba,kamanda Wakulyamba alisema wazee
na vijana ambao wanaendesha bodaboda na bajaji ni vyema wakaheshimu kazi hiyo
kama ilivyo kwa zile zinazofanyika ofisini badala ya kujihusisha na vitendo vya
kusafirisha biashara haramu na zile za magendo na hivyo kusuguana na polisi.
Licha uya kuyasema hayo kamanda,Wakulyamba alisema,usafiri
wa bajaji na bodaboda umerasimishwa na bunge la Jamhuri ya muungamno wa
Tanzania lengo likiwa kuwawezesha wananchi kupata kipato halali na kuendesha
maisha yao na kwamba kwa hatua hiyo haitakuwa vyema kuchezea kazi hiyo.
Aidha amesisitiza uzingatia sheria za barabarani kwa
madereva bodaboda kuvaa kofia ngumi huku wakiepuka kubeba abiria kwa mtindo wa
mshikaki mambo ambayo yanaweza kusababisha ajali na madhara mengine ambapo
amewahimiza watumiaji hao wa vyombo vya moto kuanza kujitambua.
“Sio vyema usafiri huu ukatumika kusafirisha biashara haramu
ama zile za magendo na ingependeza kama kazi hii mngeiheshimu kama ilivyo kazi
za maofisini kwa vile ilirasimishwa na bunge letu ili kuweza kuwaingizia kipato
halali,haitapendeza mkavunja sheria na kuanza kukimbizana na polisi”alisema.
Wakulyamba ametoa rai kwa bodaboda hao kutokuruhusu watu
wengine kuichezea kazi yao huku akiyataja makosa yanaongoza kukamatwa kuwa ni
kutokuvaa kofia ngumu ‘Helmenti’,kubeba abiria kwa mtindo wa mshikaki makosa
ambayo imegundulika kuwa wanayafahamu kabla hata ya kukamatwa.
Kamanda huyo wa polisi pia alitumia fursa hiyo kuwaasa
vijana kuacha kukaa vijiweni bila kazi huku wakikata tama za maisha na
kujihusisha na vitendo vya uhalifu badala yake wajishughulishe na shughuli
mbalimbali akitolea mfano wa kilimo hatua ambayo itawasaidia katika kumudu
kujikwamua kiuchumi.
Pamoja na wito huo kwa vijana kamanda huyo amesema kuwa
jeshi la polisi litaendelea kuimarisha vikundi vya ulinzi shirikishi jamii kwenye
maeneo mbalimbali na kufanya doria za mara kwa mara lengo likiwa kudhibiti
vitendo vya uhalifu huku akiwasihi vijana kujilinda dhidi ya vitendo vya
uhalifu.
Naye mkaguzi mkuu wa polisi kitengo cha usalama barabarani
wilayani Muheza,Herbert Kazonde amesema,changamoto kubwa iliyopo ni juu ya
vijana hao kutokujiunga na vikundi vya bodaboda hivyo kuchangia uwepo wa makosa
madogo madogo yapatayo 323 yaliyoweza kukusanywa sh 11.1 milioni.
Vilevile mkufunzi mwakilishi wa mafunzo hayo ya bodaboda
kutoka APEC Jijini Dar es salaam,Masalu Ruge alisema kwamba lengo la mafuzno
hayo ni kuhakikisha madereva wa bodaboda wanapata uelewa wa sheria kwa
kuandaliwa na GEPF mfuko wa mafao ya kustaafu.
Mwisho.
Pichani ni baadhi ya waendesha bodaboda wilayani Muheza wakiwafuatilia kamanda wa polisi mkoa wa Tanga,ambapo aliwataka kuitumia kazi hiyo kama ajira na kuacha kuitumia kufanya kazi haramu ikiwemo za magendo.
Pichani ambaye amevaa sare ya polisi na amesimama ni mkaguzi wa msaidizi wa polisi na mkuu wa kitengo cha usalama barabarani wilayani Muheza,Herbert Kazonde awali akielezea changamoto iliyopo ni vijana kuto kujiunga na vikundi vya bodaboda na kusababisha makosa madogo dogo 323 ya uvunjifu wa sheria.
Pichani ambaye amesimama ni kaimu mkuu wa kituo wilaya ya Muheza,Oscar Jeshua akizungumzia mikakati iliyopo ili kukabiliana na uhalifu ikiwemo madereva wanaovunja sheria ya usalama barabarani,katikati ni kamanda wa polisi mkoa huo,Wakulyamba na kulia ni mkuu wa wa kitengo cha usalama barabarani,Sisiwaya.
No comments:
Post a Comment