Sunday, 12 November 2017

UZINDUZI WA KAMPENI UCHAGUZI MDOGO KITI CHA UDIWANI KATA YA MAJENGO WILAYANI KOROGWE CHAMA CHA MAPINDUZI ILIKUWA HIVI,,,

 Pichani ni mapokezi ya mbunge wa jimbo la Mtera,Livingstone Lusinde juzi katika uzinduzi kampeni za Udiwani za chama cha mapinduzi CCM katika uchaguzi mdogo utakaofanyika hapo Novemba 26 mwaka huu.
 Pichani katikati ambaye ameshika kofoa ni wanachama wa chama cha mapinduzi wakimpokea mgombea udiwani wa kata hiyo ya Majengo Mustapher Sadick Shengwatu.
 M
NA SOPHIA WAKATI,KOROGWE
CHAMA cha mapinduzi CCM kimezindua kampeni zake za Udiwani katika uchaguzi mdogo utakaofanyika hapo Novemba 26 mwaka huu ambapo mbunge wa Mtera Livingstone Lusinde aliwataka wananchi wa kata ya Majengo Korogwe mjini kumchagua mgombea wa CCM  ili kuweza kuharakisha maendeleo yao.

Lusinde maarufu kwa jina la ‘Kibajaji’ aliyasema hayo juzi katika viwanja vya Sabasaba kwenye ufunguzi wa kampeni za CCM ambapo aliwaeleza wananchi kuwa amekuja Korogwe kwa ajili ya kuwasihi kumchagua mwanaCCM ambaye anaamini ndiye mgombea sahihi atakayeshirikiana na Serikali iliyopo madarakani.

Katika hotuba yake mbunge huyo wa jimbo la Mtera,alisema maendeleo ya kata ya Majengo yataletwa na wananchi wenyewe kwa kushirikiana na serikali iliyopo madarakani na kamwe jamii haipaswi kudanganyika kuchagua mgombea kutoka vyama vingine vyenye tabia ya kugomea kazi  za maendeleo.

“Ndugu zangu mimi nimekuja kuwaasa,mchagueni mgombea anayetoka CCM Mustapher Shengwatu ambapo mtaharakisha maendeleo kwa vile anapo mahali kwa kuwasilisha kero zenu ila hawa ambao wamekuwa na tabia ya kusema kuwa mkinichagua hamtashiriki kazi fulani achaneni nao”alisema mbunge Lusinde.

Mbunge huyo aliendelea kusema kuwa kuchaguliwa kwa mgombea udiwani huyo Shengwatu kutatoa fursa kwake na chama cha mapinduzi kuisimamia serikali kikamilifu hatua ambayo itawezesha utekelezwaji wa miradi mingi ya maendeleo na hivyo kata ya Majengo kusonga mbele kwa haraka.

Awali akizungumza kabla ya Lusinde aliyekuwa mgeni rasmi ufunguzi huo wa kampeni,mbunge wa jimbo la Korogwe mjini Mary Pius Chatanda alisema,wananchi hawapaswi kudanganyika na kauli za wapizani kwamba CCM haijafanya chochote huku wakitumia mitandao ya jamii kueneza propaganda hizo.

Chatanda alisema kwamba uongozi wake kwa kushirikiana na chama cha mapinduzi kupitia serikali iliyopo madarakani umefanikiwa kufanya mambo kadhaa ambayo yataleta ukombozi mkubwa kwa wananchi mjini Korogwe ambapo alisema kunajengwa mradi mkubwa wa maji kuondosha kero iliopo.

Chatanda alisema kwamba mradi huo unatekelezwa katika eneo la Mtonga na unatarajiwa kukamilika kipindi kifupi kijacho na pindi utakapokamilika unatarajiwa kuondoa kero ya maji huku idadi kubwa ya wananchi wa Korogwe wakitarajiwa kunufaika na uwepo wa mradi huo utakaokuwa wa kihistoria.

Mbali na kutaja mradi wa maji alisema kuwa jitihada zinaendelea kuboresha miundombinu ya barabara sanjari na vituo vya afya lengo likiwa kuhakikisha kwamba wananchi wanapata huduma bora ambapo aliwasisistiza wananchi wa kata ya Majengo kumchagua mgombea wa CCM ili kuharakisha maendeleo.

Naye mgombea udiwani wa kata hiyo ya Majengo Mustapher Sadick Shengwatu alisema kwamba iwapo atapata fursa ya kuchaguliwa kuwaongoza wananchi wa Majengo atahakikisha kwamba miradi yote iliyoanza kutekelezw3a inamalizika na mipya inaibuliwa kwa lengo la kutatua kero zinazoikabili jamii.

Shengwatu alisema kwamba,akichaguliwa atashirikiana vyema na wananchi bila kujali itikadi za namna yeyote ile huku akitanabaisha kuwa ataimarisha mshikamano na viongozi waliopo,wananchi katika kuisogeza mbele kata ya Mjengo huku akiahidi wanawake na vijana kuangaliwa kwa namna yake.
Mwisho.
Pichani ni mgombea kiti cha udiwani wa kata hiyo ya Majengo Mustapher Sadick Shengwatu juzi mara ya baada ya mkutano akizungumza na waandishi wa habari hawapo pichani lengo la kuwania nafasi hiyo.

No comments:

Post a Comment