NA SOPHIA WAKATI,MUHEZA
MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Muheza mkoani Tanga, Naima Bakari Chondo, amewakaribisha wadau, hususan wakulima, kutembelea wilaya hiyo ili kutumia fursa zilizopo katika sekta ya kilimo kuongeza uzalishaji.
Chondo amesema wilaya ya Muheza ina ardhi yenye rutuba na hali nzuri ya hewa, ambazo ni miongoni mwa fursa zinazoweza kutumiwa na wakulima kuongeza uzalishaji wa mazao mbalimbali ya nafaka.
Ametoa wito huo wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani Kitaifa yaliyofanyika Viwanja vya Usagara vilivyopo jijini Tanga, ambapo Halmashauri ya Wilaya ya Muheza iliweza kushiriki kwa kuweka banda la maonesho.
Kauli mbiu ya Siku ya chakula duniani Kitaifa kwa mwaka huu inasema" ubunifu wa leo lishe bora ya kesho kuelekea Dira 2050".
Alizungumzia zaidi sekta ya Kilimo, Mkurugenzi huyo alisema kuwa,anajivunia nafasi ya Muheza katika uzalishaji wa mazao ya viungo na kusisitiza kuwa wilaya hiyo ina fursa zinazoweza kuvutia wadau zaidi kuwekeza katika kilimo cha mazao ya aina mbalimbali.
Chondo pia ameeleza kufurahishwa na ushindi uliopatikana na halmashauri hiyo katika maadhimisho hayo, akisema ilistahili kupata tuzo hiyo.
Amesisitiza kuwa matumizi ya fursa zilizopo katika sekta ya kilimo yanaweza kuwawezesha wakulima kuongeza uzalishaji na kunufaika zaidi na shughuli zao.
Maadhimisho hayo yalifungwa Oktoba 16, 2026, na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dk. Batilda Salha Burian, aliyemwakilisha Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Balozi Dk. Bashiru Ally Kakurwa.
Mwisho.




No comments:
Post a Comment