![]() |
| Picha ni Mkuu wa Jimbo la Pwani,Issay Amasia Mweta katika ibada akiwataka waumini kujenga moyo wa kufurahia mafanikio. |
NA SOPHIA WAKATI,,TANHA
MKUU wa Jimbo la Pwani Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Issay Amasia Mweta, amewataka waumini na jamii kujenga moyo wa kufurahia mafanikio ya wengine, akisema tabia hiyo ni miongoni mwa misingi muhimu ya kufanikiwa katika maisha.
Akizungumza jumapili wakati wa ibada katika Kanisa la KKKT Kana, jijini Tanga, Mweta alisema mtu anayetaka kufanikiwa anapaswa kujifunza kufurahia mafanikio ya wengine badala ya kuwa na moyo wa kutoridhika wanapopiga hatua za maendeleo.
Alisema tabia ya kutofurahia mafanikio ya wengine ni kikwazo kinachoweza kumwingiza mwanadamu katika mazingira ya kukosa mafanikio, hivyo ni muhimu kuachana na roho hiyo na kujenga moyo wa upendo na kuthaminiana.
Mchungaji Mweta alisisitiza kuwa roho ya tabia isiyofaa haipaswi kuwa sehemu ya maisha ya mwanadamu, akiwataka waumini kuacha kulaumu uumbaji wa Mungu na badala yake kujitathmini katika mwenendo wao wa kila siku.
Alieleza kuwa kumtumikia Mungu si jambo linalopaswa kusubiri mtu ahubiriwe au akumbushwe kila wakati, bali ni wajibu wa mtu binafsi kuamua kumtumikia Mungu kwa moyo wake na kwa vitendo.
Aidha, aligusia suala la kutoa mavuno, akisisitiza kuwa uwajibikaji huo unatokana na mtu mwenyewe na moyo wake wa kumshukuru Mungu, huku akitofautisha utoaji wa sadaka ya ujenzi na sadaka ya mavuno.
Katika ibada hiyo, waumini walishiriki na kuhamasishwa kuchangia sadaka kwa ajili ya ujenzi , huku wakielezwa kuwa sadaka hiyo ni tofauti na sadaka ya mavuno ambayo muda wake ulikuwa bado haujafika.
Alifafanua kuwa Novemba 8 ndiyo siku iliyopangwa kwa ajili ya Sikukuu ya Mavuno, hivyo waumini walikumbushwa kuzingatia utofauti wa sadaka hizo na nyakati zake.
Katika mafundisho yake, Mweta pia alisimulia hadithi ya Sandalati na Tobia, akitumia kisa cha mkuyu na boga kutoa mafunzo yaliyolenga kuwajenga waumini katika mtazamo wa maisha na imani.
Kwa ujumla, ujumbe wake uliweka msisitizo katika imani, kujitathmini, kumtumikia Mungu kwa moyo wa hiari na kuwa na moyo wa kufurahia mafanikio ya wengine kama sehemu ya kujenga maisha yenye upendo na mafanikio.
Mwisho.

No comments:
Post a Comment